RAIS SAMIA AONESHA FURAHA ASAFIRISHA ABIRIA RELI SGR BILA MALIPO


Baadhi ya abiria wakiwa ndani ya treni ya mwendo kasi (SGR) tayari kwa kuanza safari   ya kurejea jijini Dar es salaam baada ya kufika mkoani Morogoro ikiwa ni kusheherekea safari ya kwanza ya treni hiyo.
Baadhi ya abiria wakishuka kwenye treni ya kisasa ya mwendo kasi mara baada ya kuwasili kwenye kituo cha Morogoro wakitokea Dar es salaam. (Picha zote na Christina Cosmas, Morogoro)

Na Christina Cosmas, Morogoro

RAIS Samia Suluhu Hassan ameonesha furaha yake kwa kuwalipia nauli abiria zaidi ya 1400 wa mwanzo wa treni ya kisasa ya mwendo kasi (SGR) waliosafiri kutoka Jijini Dar es salaam – Morogoro - Dar es salaam kama ishara ya kusherehekea uzinduzi wa safari hizo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ambaye alikuwa miongoni mwa wasafiri wa reli hiyo alisema hayo jana baada ya kuwasili na treni ya kisasa ya mwendo kasi katika kituo cha Morogoro ikiwa ni mwanzo wa usafiri huo wa kufanya safari zake katika kutoka Dar es salaam hadi Morogoro kwa umbali wa kilometa 300 kwa kutumia saa 1:45.

“reli hii ni faida kwa wananchi wetu, kutoka Dar es salaam treni hii waliyokuja nayo ni shilingi 13,000 ambayo mwananchi wa kawaida anaiweza na kwenda mpaka Dodoma ni shilingi 30,000 mwananchi anaweza kuwahi na akaenda kufanya shughuli zake na kurudi alipotoka” alisema Kihenzile.

Akizungumzia hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa alisema watanzania wengi walilisubiri jambo hilo kwa hamu kwa kuona jambo hilo ni la ukweli au laa na sasa wamehakikisha ni la ukweli.

Kadogosa alisema hilo ni jambo la furaha na kubwa kwa Taifa na Watanzania wana haki ya kujivunia na kutumia fursa hiyo sababu mambo hayo inawezekana wakayaona ya kawaida lakini si mambo ambayo yanatokea katika nchi zingine.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRC Ally Kalavina aliwaomba watanzania kuzingatia muda wakati wa kupata huduma hiyo sababu inakwenda na muda uliopangwa tofauti na usafiri mwingine ikiwemo treni iliyozoeleka ya reli ya kati.

Naye Mmoja wa Abiria waliopanda treni kutoka Morogoro- Dar es salaam Inda Saidi Mhando alisema usafiri wa treni anaotumia umemuhamasisha kusafiri zaidi kwa kutumia reli sababu unahamaisha utalii wa ndani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post