SERIKALI YAZINDUA CHUMBA CHA UFUATILIAJI MWENENDO WA MAJANGA NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Joakim Mhagama akizungumza kwenye uzinduzi wa Chumba maalum cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kilichopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma leo June 14,2024.
Na Dotto Kwilasa,Malunde Blog 1,DODOMA.

Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)imezinduzi Chumba maalum cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kilichopo Mji wa Serikali  Mtumba, Dodoma kitakacho imarisha upatikanaji wa taarifa za uwezekano wa kutokea kwa majanga na tahadhari za mapema kwa wanajamii wote na taasisi mbalimbali .
Akizungumza kwenye uzinduzi huo leo June 14,2024 Jijini Dodoma,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Joakim Mhagama amesema humba hicho  kimeanzishwa ikiwa ni sehemu ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura na kutarajiwa kuimarisha operesheni za majanga kwa kuunganisha vituo mbalimbali vya kisekta, Kituo cha kikanda vya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Kituo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kituo cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

 "Chumba hiki  kimefungwa vifaa mbalimbali vya TEHAMA pamoja na mifumo mbalimbali ya kufuatilia mwenendo wa majanga na tahadhari ya mapema ikijumuisha jukwaa la ki-eletroniki la myDEWETRA ambalo limeunganisha taarifa za kijiografia kwa ajili ya uchambuzi wa utabiri wa hali ya hewa na haidrolojia hatarishi ya mafuriko, ukame, vimbunga, Tsunami na upepo mkali ili kuweza kufanya tathmini ya madhara na kutoa tahadhari ya mapema kwa wakati na eneo husika,"ameeleza. 

Mhagama pia ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wataalam wote  watakaopangiwa kufanya kazi katika chumba hicho kuhakikisha kuwa shughuli zilizopangwa kufanyika zinatekelezwa kwa ufanisi ili kuhakikisha taarifa za tahadhari za mapema zinawafikia walengwa kwa wakati hasa wanajamii na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga. 

Amesema mafanikio hayo yametokana  na mradi ulioanzishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na  kufadhiliwa na Serikali ya Nchi ya Italia kupitia Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia kutoa utaalamu wa utekelezaji wa shughuli zote.  
"Katika kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya maafa, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 Ibara ya 107 pamoja na miongozo mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa ya utekelezaji wa hatua za usimamizi wa maafa, "amesema

Amesema kupitia majanga mbalimbali yaliyotokea nchini na athari zilizotokea, Serikali imeona umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za awali na ufuatiliaji wa majanga kwa kuanzisha chumba chenye vifaa na mifumo ya kisasa kwa ajili ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga mbalimbali na uchukuaji wa hatua za mapema. 

"Napenda kutumia pia fursa hii kutambua mchango wa utaalamu na takwimu mbalimbali zilizotolewa na Wizara ya Maji na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambazo zimesaidia katika uanzishaji wa mifumo ya ufuatiliaji wa majanga iliyopo katika chumba cha Ufuatiliaji wa majanga, "amesema

Amefafanua kuwa jumla ya wataalamu 27 wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu mifumo itakayotumika kwenye chumba cha ufuatiliaji wa majanga na utoaji wa tahadhari za awali ambapo kati ya hao, (8) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, (14) kutoka Wizara ya Maji na (5) kutoka Malmaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Aidha wataalamu sita (6) kati ya waliopata mafunzo wameainishwa kuwa watatekeleza shughuli za ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na utoaji wa tahadhari za mapema na uchukuaji wa hatua za haraka katika chumba hicho. 
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt.Jim Yonazi ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi na kwamba katika kutekeleza hilo, imeshiriki katika utekelezaji wa mradi wa uanzishaji wa Chumba cha Ufuatiliaji wa Majanga na Tahadhari za Mapema ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa jukwaa la kieletroniki lijulikanalo kama myDEWETRA. 

Amefafanua kuwa uanzishaji wa chumba cha ufuatiliaji wa majanga ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema nchini na kufafanua kuwa kimeanzishwa ikiwa ni sehemu ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kwa lengo la ufuatiliaji wa uwezekano wa utokeaji wa majanga na kutoa tahadhari ya mapema ili kuweza kuchukua hatua za mapema za kuzuia, kupunguza na kujiandaa kukabiliana na maafa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa uanzishwaji wa chumba hicho,Dkt.Yonazi ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilitekeleza jukumu la kuratibu ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika na taasisi CIMA Research Foundation ya Italia katika uanzishwaji wa chumba hiki cha ufuatiliaji wa majanga na uundaji wa jukwaa la kielektroniki lijulikanalo ka myDEWATRA. 

"myDEWETRA ni mfumo unaotumika kufuatilia, kuchambua na kuratibu taarifa na takwimu za majanga, hali ya uwezekano wa kuathirika, utabiri wa hali ya hewa na haidrolojia hatarishi na uchambuzi wa madhara yanayoweza kutokea, " amefafanua Katibu Mkuu huyo .

"Kwa msingi huo, Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu Mfumo wa Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote ambao umezingatia utekelezaji wa hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, na kujiandaa kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea. Mfumo umezingatia kila sekta kutekeleza wajibu katika eneo lake ambalo imepewa jukumu la Kisera na Kisheria kwa kutumia rasilimali zilizopo kwa kushirikiana na wadau wengine, "amefafanua na kueleza;
Licha ya hayo Mradi wa uundaji wa jukwaa hili tumeufanya kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa katika Kanda ya Afrika (United Nations Office for Disaster Risk Reduction Regional Office for Africa) kwa ufadhili wa Serikali ya Italia kupitia Shirika la Maendeleo la Italia na kutekelezwa na Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia, "amesisitiza .

Dkt. Yonazi ameyataja majukumu ya chumba hicho kuwa ni kufanya ufuatiliaji wa uwezekano wa kutokea kwa majanga kwa kutumia mifumo ya kiteknolojia ya kijiografia na haidrolojia iliyopo ikiwemo jukwaa la kielektroniki la MyDEWETRA;kufuatilia mwenendo wa janga lililotabiriwa na kufanya uchambuzi wa kiwango cha madhara kwa jamii, miundombinu na mazingira. 

Mengine ni uandaaji wa taarifa za tahadhari ya mapema na hatua za kuchukua ili kuzuia, kujiandaa na kukabili janga,kusambaza taarifa za tahadhari ya mapema na hatua za kuchukua kwa jamii na wadau mbalimbali,kuandaa taarifa ya mwenendo wa tukio (situation report) na kusambaza wadau mbalimbali kwa ajili ya kusaidia uratibu na utekelezaji wa shughuli za kukabili na kurejesha hali. 

Naye Naibu Katibu Mkuu anayemuwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR) Marco Riccardo Rusconi ameeleza kuwa uzinduzi huo utasaidia kushirikiana na vituo vya kikanda na kimataifa vinavyosimamiwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika ili kuboresha udhibiti wa maafa yanayovuka mipaka. 

Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation -AICS) Prof. Eng. Luca Ferraris amesema uanzishwaji wa Chumba hicho umezingatia hatua za kuchukuliwa na kila sekta zinazohusika katika ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na utoaji wa tahadhari ya mapema ili kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kwa kuzingatia uwajibikaji wa pamoja ambapo.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post