Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza Tanzania CP Nicodemus Menyamsumba Tenga akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza katka masuala ya huduma za msaada wa kisheria leo juni 12 Jijini Arusha.
Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Bi. Ester Msambazi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza katka masuala ya huduma za msaada wa kisheria leo juni 12 Jijini Arusha.
Na Imma Msumba ; Arusha
Kamishna wa Sheria na uendeshaji wa Magereza Nchini CP Nicodemus Menyamsumba Tenga amewataka Maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza nchini kuhakikisha wanasimamia haki zote za binadamu katika maeneo yao ya kazi.
Cp Tenga ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza katika masuala ya huduma za msaada wa kisheria yanayoendelea jijini arusha kwa siku mbili.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria, Mgeni Rasmi CP Nicodemus Menyamsumba Tenga amewataka maafisa hao kwenda kutekeleza majukumu yao mahususi mara wamalizapo mafunzo hayo ili yakawe na tija na matokeo mazuri ya utoaji haki.
“Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha watanzania wanapata haki, pamoja na kunufaika na uwepo wa mifumo ya kijinai ya uhakika kwa kuimarisha miundombinu ya utoaji haki na watoa haki za kijinai hapa nchini” Alisema Cp Kamishna Tenga.
Hata hivyo aliongezea kuwa wao kama majeshi ya kulinda haki hawatamuangusha Rais Samia bali wataendelea kutembea na maono ya Rais ili kuhakikisha katika Taasisi zote wanazosimamia wananchi wanakwenda kupata haki zao za kimsingi na sio kukiuka haki za binadamu.
Mbali na hilo Kamishna Cp Tenga ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria kuhakikisha hawaishii kutoa mafunzo kwa viongozi wa juu tu bali waendelee kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali ambayo yanasimamia Haki za binadamu katika Taasisi mbalimbali za Kijinai ili kuweza kupata matokeo mazuri katika utoaji haki.
Kwa upande wake Msajili wa watoa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi amewataka maafisa hao kuendelea kusimama kwa pamoja ili kuhakikisha haki za wananchi zinapatikana kwa wakati na sehemu yoyote kwani serikali imeboresha maeneo mbalimbali ya huduma za kisheria.
“Tunalishukuru sana Jeshi la Polisi na Magereza kwa ushirikiano wao mkubwa sana katika Wizara yetu kwani katika masuala yetu ya msaada wa kisheria wamekuwa wadau wakubwa sana katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa ufanisi” Alisema Bi. Ester Msambazi.
Bi. Veronica Sigalla akimwakilisha Mkurugenzi mkazi wa UNDP hapa nchini amelishukuru Jeshi la Magereza kwa kazi kubwa wanayofanya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kupunguza kasi kubwa ya malalamiko ya ukiukwaji wa Haki za binadamu kwani bila uongozi mzuri na dhabiti lisingewezekana,pia amewaomba maafisa hao kuendelee kuunga mkono jitihada za kiserikali ili kuhakikisha msaada wa kisheria unaendelea kutolewa.
Social Plugin