JAMII imetakiwa kutilia mkazo ushiriki wa watoto katika michezo mbalimbali ili kuwajengea uwezo na kukuza ujuzi wa sitadi za maisha ktika kukabiliana na vikwazo mbalimbali ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia.
Hayo yameelezwa na wadau katika kongamano la mashindano ya riadha kwa wanafunzi wa skuli mbalimbali za Zanzibar yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Idara ya Michezo, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Taasisi ya Maendeleo ya Mashirikiano ya Ujerumani (GIZ) na Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD) kwa lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia katika michezo.
Akizungumzia juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhamasisha michezo kwa maendeleo, Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuhamasisha michezo kwa wote ili kukuza ushiriki wa jinsi zote katika michezo.
"Tuwe mifano mizuri ya kuwa na heshima katika jamii, kwasababu sisi tuna nafasi ya kupata mawaidha sehemu mbalimbali ya stadi za maisha. Hivyo tuna kila sababu ya kuendeleza kuimarisha na kuhamasisha michezo kwa wote," alisema Dkt. Issa.
Kwa upande wake, Wanu Ali Makame, Meneja Idara ya Mitaala na Vifaa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, alibainisha kuwa katika kutilia mkazo umuhimu wa Michezo kwa Maendeleo, wizara imeweka somo maalum linaloelezea masuala ya Michezo.
Alieleza, “tuna somo maalum linaloelezea masuala ya Michezo Kwa Maendeleo. Tunaweza tukacheza na tukasoma kwa salama na amani bila kuathiri hulka na tabia ya mtu yeyote yule aliyetuzunguka.”
Hija Ramadhan kutoka Shirika la GIZ aliongeza kuwa jitihada za kutengeneza usawa wa kijinsia ni pamoja na kuhakikisha waadau wanashirikiana kuwalinda watoto na wanawake dhidi ya ukatili.
"Lengo hili tunaweza kulifikia kwa kutumia mbinu tofauti ikiwemo Michezo kwa Maendeleo," alisema Ramadhan.
Katika hafla hiyo hayo wanafunzi walipata fursa ya kushiriki mbio fupi na washindi kuzawadiwa zawadi mbalimbali ikiwemo medali na madaftari ya kusomea.
Mashindano hayo yamewaleta pamoja wadau mbalimbali ikiwemo wanafunzi kutoka skuli za Unguja, wanamichezo, walimu wa michezo, na wadau wa masuala ya usawa wa kijinsia yakiambatana na kaulimbiu “Wakati ni sasa! Wekeza katika elimu na michezo kwa watoto wote”, ikiwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha michezo inatumika kama chombo cha kuleta maendeleo na usawa katika jamii.
Social Plugin