Na Mwandishi Wetu, Kigoma
BIDHAA za aina mbalimbali zenye thamani zaidi ya sh.milioni 34 zimeteketezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi Kigoma baada ya kukamatwa kupitia ukaguzi uliofanywa na maofisa wa TBS kwa kipindi cha kati Julai 2023 hadi Mei 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Kigoma wakati wa kuteketeza bidhaa hizo zenye uzito wa tani tani 3.6, Afisa Udhibiti Ubora wa TBS Kanda ya Magharibi, Elisha Meshack, alisema ukaguzi huo ulifanyika ili kuhakikisha TBS inaondoa sokoni bidhaa hafifu ili kulinda usalama wa watumiaji wa bidhaa hizo
Alitaja miongoni mwa bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na zile zilizopigwa marufuku kutumika hapa nchini ikiwemo vipodozi vyenye viambata sumu na nguo za ndani za mitumba.
Bidhaa nyingine ni nyaya za umeme zilizo na rangi zilizopigwa marufuku pamoja bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi ambazo zilikamatwa katika kaguzi maalumu na za kawaida ndani ya Halmshauri za Mkoa wa Kigoma ikiwemo Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kasulu Mji, Kibondo na Kakonko.
Meshack alisema nguo za ndani zimepigwa marufuku kwa sababu zinasababisha maradhi ya ngozi kama vile fangasi na maambukizi ya bakteria yanayopelekea magonjwa ya ngozi kwenye maeneo mbalimbali za mwili
Kwa upande wa vipodozi, vyenye viambata sumu, alisema husababisha kuathirika kwa mifumo ya uzazi kwa wanawake na wanaume, kuharibika kwa ngozi, kusababisha madhara kwa mtoto anaenyonyeshwa na aliyepo tumboni, kusababisha saratani za aina mbalimbali ikiwemo ya ngozi na kuathirika kwa mifumo wa umeng'enyaji wa chakula.
Alisema vipodozi vilivyoteketezwa vimepigwa marufuku katika soko la Tanzania kwa sababu vina viambata sumu ikiwemo hydroquinone, butylmethyl propional, steroids, zinc pyrothione na zebaki. ALitaja madhara ya rangi za nyaya za umeme ni kuharibika kwa vifaa vya umeme vya watumiaji wa vifaa hivyo ikiwemo kuwa chanzo cha ajali za umeme zinazosababisha majeruhi watu kuumia au kifo
Alisisitiza wananchi kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa wanazotaka kununua ili kujua kama hazijaisha muda wake wa matumizi na kama zimethibitishwa na TBS.
Ili kuepuka kadhia , alitoa rai kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha kuwa wanaingiza sokoni bidhaa zenye ubora.
"Rai yetu ni kuwa wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa kufuata kanuni, taratibu na Sheria ili kuepuka kupata hasara na kuchukuliwa hatua za kisheria. Ni vema wakawa wanawasiliana na Shirika la Viwango kwa kufika ofisi za TBS zilizo karibu nao au kwa mifumo yetu ya mtandaoni au kwa kupiga simu ya bure 0800110827 ili waweze kupewa maelezo au msaada,: alisema Meshack.
Social Plugin