Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YATEKETEZA TANI 7.2 ZA BIDHAA HAFIFU KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI


Na Mwandishi Wetu, Mbeya

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini limeteketeza tani 7.2 za bidhaa hafifu zikiwemo zilizoisha muda wake wa matumizi vikiwemo vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 43.

Miongoni vya bidhaa zilizoteketezwa ni vipodozi vyenye viambata sumu ambavyo vimepigwa marufuku kutumika nchini, vinywaji vyenye vilevi vilivyoisha muda wake wa matumizi (Bia, Mvinyo), juisi, soda, vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drink), mafuta ya kula, biskuti, maziwa ya watoto, tomato na chili sauce, blue band na bidhaa zingine mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya leo wakati wa kuteketeza bidhaa hizo, Meneja wa TBS, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Abel Mwakasonda, amesema bidhaa hizo zilikamatwa katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Juni, mwaka huu kufuatia ukaguzi uliofanyika katika halmashauri za Mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa.

Alitaja bidhaa za vipodozi zilizoteketezwa kutokana na kupigwa marufuku katika soko la Tanzania ni vile venye viambata sumu venye madini kama Zebaki (Mercury), madini Tembo (Lead) na Hydroquinone.

Alisema bidhaa hafifu vilivyoteketezwa pamoja na vipodozi pindi vinavyotumiwa na watumiaji vinasababisha madhara mbalimbali ya kiafya. Miongoni mwa madhara ya kiafya yanayosababishwa na bidhaa hizo kwa mujibu wa Mwakasonga ni magonjwa ya matumbo, saratani ambapo vipodozi hivyo vinaondoa asili ya ngozi pamoja na kusababisha madhara mengine mbalimbali katika mwili wa binadamu.

Alitoa rai kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha kuwa wanaingiza sokoni bidhaa ambazo zimethibitisha ubora wake na TBS, vinginevyo zitaondolewa sokoni na kuteketezwa kwa gharama zao wenyewe.

Kwa mujibu wa sheria ya viwango ni marufuku kwa wazalishaji, wazambazaji na wauzaji kuingiza kwenye soko la Tanzania bidhaa ambazo hazijathibitishwa ubora wake na TBS.

Mwakasonda, alisema ukaguzi wa bidhaa sokoni unafanywa kwa kuzingatia Sheria ya Viwango Na:2 ya mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2021 sambamba na Sheria ya Fedha namba Na: 8 ya mwaka 2019.

Aidha, Mwakasonda aliwataka wananchi kutotumia bidhaa ambazo hazijathibitishwa na TBS zikiwemo zile zilizopigwa marufuku kutumika nchini vikiwemo vipodozi vyenye viambata sumu.

Alisisitiza wananchi kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa wanazotaka kununua ili kujua kama hazijaisha muda wake wa matumizi na kama zimethibitishwa na TBS.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com