Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi, akizungumza wakati wa kikao na wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini ili kuzalisha chakula bora na chenye tija, kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Na. Edward Kondela - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Serikali imeanza kufanya kazi kwa karibu na vyama vya mifugo nchini kupitia vikao mbalimbali ili kuhakikisha usalama na ubora wa vyakula vya mifugo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, mara baada ya kufanya kikao na wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini ili kuzalisha chakula bora na chenye tija.
Dkt. Bitanyi amesema kuwa serikali itahakikisha inasimamia suala la ubora na wakala hiyo itakuwa na mikutano ya mara kwa mara pamoja na kutoa elimu na kutembelea maeneo yanayotengenezwa vyakula vya mifugo na kusimamia ubora.
“Tumeanza kufanya kazi kwa karibu na vyama vya mifugo nchini na mkutano wa leo tumeanza na Chama cha Wazalishaji wa Vyakula vya Mifugo nchini (TAFMA) pamoja na vyama vingine vya ndege wa wafugwao vikao hivi vinalenga kusimamia usalama na ubora wa mifugo, maana wafugaji wadogo nchini wanategemea wazalishaji wa vyakula vya mifugo kuzalisha vyakula bora ili kuongeza tija kwa wafugaji na wapate matokeo mazuri ya mifugo yao.” Amesema Dkt. Bitanyi
Kwa upande wao baadhi ya wadau waliohudhuria kikao hicho, wamepata nafasi ya kutoa maoni yao pamoja na kutaka ufafanuzi wa baadhi ya majukumu ya TVLA na kuomba uwepo wa vikao vya mara kwa mara ili kuwakumbusha wazalishaji wa vyakula vya mifugo kuzalisha vyakula bora.
Wamesema wananufaika na elimu ambayo inatolewa na TVLA pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyakula vya mifugo nchini ili kuhakikisha wafugaji wanapata vyakula bora na hatimaye kufikia malengo ya ufufgaji wao.
TVLA inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.
Baadhi ya wadau kutoka vyama vya mifugo nchini wakiwa kwenye kikao kilichoitishwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) kujadili mustakbali wa kupata vyakula bora vya mifugo ili viwe na tija kwa wafugaji. Kikao hicho kimefanyika makao makuu ya TVLA jijini Dar es Salaam.