UMOJA WA ULAYA, UNCDF WAIUNGA MKONO SERIKALI KUFIKIA MALENGO YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Na Mwandishi Wetu

Katika kufikia malengo ya mwaka 2034 ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi, wadau wametoa wito wa kutolewa elimu ya kutosha Kwa jamii mijini na vijijini ili kufikia malengo hayo kwa haraka.

Hayo yamesemwa na wadau katika Kongamano la wadau wa nishati safi kwa ajili ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa miaka 10 liloandaliwa na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa ( UNCDF) kwa siku tatu katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Katika kongamano hilo wa wadau wamesema utekelezaji wa ajenda ya nishati Safi utakuwa na mafanikio kwa sababu licha ya jitihada kubwa za serikali na wadau, una utashi mkubwa ulioyeshwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Meneja wa Mradi wa mradi wa Cookfund unaosimamiwa na UNCDF Imanuel Muro amesema kuwa katika kufikia malengo ya mradi huo ni pamoja na kutoa elimu katika ngazi zote juu ya uhamasishaji wa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ikiwemo Teknolojia ya Mkaa mbadala na Nishati nyinginezo ambazo hazitokani na ukataji Miti, uchafuzi wa mazingira na hatarishi kwa afya ya binadamu, wakiwemo wanawake na akina mama ambao kwa kiasi kikubwa wanatumia muda mwingi katika mapishi kwa familia.

Muro amesema kuwa katika kufikisha elimu wanatarajia kutoa magari mawili yatakayofanya kazi ya kutoa elimu katika ngazi zote kutoka kwa wataalaam.

Aidha amesema kuwa mwamko umeanza kwa Sekta binafsi kuwa na ubunifu wa teknolojia ya utengenezaji wa majiko ya Kupikia pamoja na Mkaa mbadala ambao ni rafiki, zinaokoa muda na kulinda mazingira.

Mkuu wa UNCDF Tanzania, Peter Malika, amesisitiza juu ya umuhimu wa kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu linawaleta wadau kwenye majukwaa hayo kujadili na kuona namna gani wanakwenda kutekeleza mradi huo.

Pia amesema kuwa UNCDF inategemea kuwa na majukwaa ya aina hiyo mikoani ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Amesema kuwa kuna umhimu kuambatanisha juhudi za kuelekea malengo endelevu ambayo yanasisitiza umuhimu wa Nishati Safi ya Kupikia ambayo itaokoa ukataji miti na kulinda afya ambapo jamii, likiwemo kundi kubwa la wanawake inaathirika na madhara mbalimbali ya moshi wa kuni.

Aidha kongamano hilo linatoa nafasi kwa ajili ya mazungumzo, ushirikiano na hatua za kuchukua ili kufikia maono sawa ili Tanzania iende sawa na mkakati huu wa kidunia.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Masoko na Teknolojia katika kubadilisha mapishi safi kwa kuzingatia mkakati wa kitaifa wa nishati safi wa 2024-2034’ una lengo la kuwaleta pamoja wadau muhimu katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia .

Program Meneja wa Nishati wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) Massimiliano Pedretti amesema kuwa walipokuwa wanaandika mradi hawakutegemea kupata mwitikio mkubwa lakini wameona mwitikio huo umeanza na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kama mkuu wa nchi ameonyesha kwenda kuleta mabadiliko.

Amesema kuwa kazi iliyopo ni kwenda kutoa elimu katika maeneo yote pamoja na kuhakikisha jamii wanakwenda kutumia Nishati Safi ya Kupikia.

Mratibu wa Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia wa Wizara Nishati Joyce Msangi amesema kuwa kazi ya Wizara ni kutengeneza Sera ya kuweza kufikia mipango ikiwemo kuangalia uwezekano wa kodi zinatozwa kupungua ili kila mwananchi awe na uwezo wa kupata Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanzia ngazi ya chini hadi juu.

Amesema kongamano hilo limetoa picha na kufanyia kazi maoni ya wadau katika kuhakikisha huo uelewa unamfikia kila mtu.

Mhandisi wa Maendeleo ya Mradi wa Watu na Umeme Egberth Bashweka amesema katika Ubunifu wao wameona njia rahisi ya nishati Safi ya Kupikia ni pamoja na matumizi ya nishati ya Umeme jua ambapo umefanya vizuri baadhi ya Taasisi kuwa na majiko ya kutumia umeme wa jua.

Amesema kuwa Umeme wa jua unapunguza gharama nyingi na kurahisha shughuli mbalimbali za maendeleo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post