Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Shirika la UNFPA Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya nchini linatarajia kutekeleza mradi wa "Thamini uzazi salama" katika wilaya 3 za Mkoa wa Shinyanga wenye lengo la kutoa elimu na ujuzi kwa watoa huduma katika vituo vya afya na zahanati hususani wakunga unaotarajia kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 22.2.
Hafla ya utambulisho wa mradi unaofadhiliwa na serikali ya Canada imefanyika leo Juni 19, 2024 katika ukumbi wa hoteli ya Vigimark uliopo manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amelipongeza shirika la UNFPA kwa kuendelea kuiunga mkono serikali na kuahidi kushirikiana na watendaji wote kuanzia ngazi ya wilaya ili kufikia malengo ya mradi huo.
"Niwapongeze sana UNFPA kwa kuendelea kuiunga mkono serikali yetu na niwaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano kwenye mradi huu na miradi mingine inayokuja, tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi bado vipo na ujio wa mradi huu kwenye halmashauri zetu utakwenda kupunguza vifo hivyo kwa sababu mradi huu umebeba dhana nzima ya elimu na utaalamu kwenda kwa wakunga na wataalamu wetu kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma", amesema RC Macha.
"Tunawashukuru wote mlioandaa mradi huu ni imani yangu ndani ya miaka saba ya utekelezaji wa mradi huu kutakuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya hapa mkoani kwetu, niwahakikishie mradi huu upo sehemu salama na sisi tunaubeba, baada ya kusema hayo niseme tu mradi huu tunaupokea na kuahidi kutekeleza kikamilifu kupitia watendaji wetu", ameongeza RC Macha.
Awali mwakilishi kutoka UNFPA Felista Bwana amesema mbali na utekelezaji wa mradi huo pia wanatarajia kufanya planning ya mradi huo ndani ya wilaya 3 za mkoa wa Shinyanga pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji na kutambua vipaumbele na sehemu zenye uhitaji mkubwa wa uzazi salama.
Mwakikishi kutoka Wizara ya Afya Satuni Manangwa ametaja vipaumbele vya mradi huo na manufaa manufaa yake kwenye jamii.
"Serikali yetu imefanya juhudi kubwa kwenye kupanua huduma za afya na sisi kama Wizara ya Afya ofisi ya Rais TAMISEMI tumeweka kipaumbele kwenye ubora wa huduma kwa mwananchi wa kawaida pamoja na kufungua huduma muambata",
"Mradi huu umetengenezwa na serikali kupitia Wizara ya Afya ofisi ya TAMISEMI ambapo katika utekelezaji wake umelenga kuwafikia wakunga, ushahidi unaonyasha kati ya kina mama 100 wakihudumiwa na mkunga aliyepatiwa elimu ya kutosha na ujuzi basi kina mama 80 wanaweza kujifungua salama bila matatizo na tunatarajia kufika kuanzia ngazi ya chuo hadi kazini", ameongeza Satuni Manangwa.