Wadau wa maji wakiwa kwenye picha ya pamoja
Katibu tawala wa mkoa wa Morogoro Dk. Musa Ally Musa (kulia) akizungumza na waandishi wa habari juu ya umuhimu wa kupanda mikarafuu kama miti ya kulinda vyanzo vya maji huku wananchi wakinufaika.
Na Christina Cosmas, Morogoro
KATIBU Tawala wa mkoa wa Morogoro Dk. Musa Ally Musa amewataka wadau wa mazingira kuzingatia suala la upandaji miti kwa ajili ya utunzaji wa vyanzo vya maji huku ukiendana na kuondoa umaskini kwa wananchi kwa kupanda miti ya mazao ya biashara.
Dk. Musa amesema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya maadili kwa menejimenti na watumishi wa bodi ya maji bonde la Wami Ruvu yanayofanyika mkoani hapa.
“tukipanda mikarafuu, maana yake ni fedha, ikipandwa 40 tuu ambayo inaingia katika heka moja ni milioni 19 mpaka 13, hizo tayari zinatosha kumtoa mtu au familia katika janga la umaskini” amesema.
Hivyo amesema mipango inayopangwa ni lazima ihusishe na suala la kuwatoa watu katika umaskini licha ya kulinda vyanzo vya maji kwa kupanda miti na kwamba wakishindwa kufanya hivyo hawataweza kufikia viwango wanavyotaka.
Anasema upandaji wa miti si tu ya vivuli bali pia hata michaichai, migomba na miparachichi nayo ni miti ambayo ni mali inayoweza kuwaondoa wananchi katika suala zima la umaskini.
Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi amesema tayari wameshapanda miti 500 ya mikarafuu katika maeneo ya mkoa wa Morogoro.
Mhandisi Mmasi anasema katika mwaka ujao wa fedha watakuwa na miti 20,000 ya mikarafuu, miti 5000 ya parachichi kutoka Njombe na migomba kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambayo itatumika na wanavijiji waliopo pembezoni mwa vyanzo vya maji baada ya kupewa elimu na kuridhia aina ya miti wanayohitaji.