Na Mwandishi Wetu, Geita
WANANCHI wamehimizwa kununua na kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na kuhakikisha bidhaa wanazotumia hazijaisha muda wake wa matumizi ili kulinda afya zao.
Ushauri huo ulitolewa na Afisa Udhibiti Ubora wa TBS, James James kwenye Maonesho ya Fahari ya Geita yaliyohudhuriwa na wajasiriamali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kwenye viwanja vya EPZA Bomba mbili, mkoani Geita.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi mbalimbali waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonesho hayo kuanzia Mei 22 hadi Juni 2, mwaka huu , James alisema TBS imekuwa ikiwakumbusha mara kwa mara wananchi kabla ya kununua bidhaa wanazohitaji wahakikishe wanasoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio ambazo zitawasaidia kujua taarifa mbalimbali za bidhaa husika ikiwemo kuthibitishwa na TBS pamoja na muda wake wa mwisho wa matumizi.
"Tunahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kusoma taarifa za bidhaa wanazotaka kununua kwenye vifungashio ili waweze kujua taarifa za msingi za bidhaa husika ikiwa ni pamoja na kuthibitishwa ubora wake na TBS," alisema James.
Aidha, kupitia maonesho hayo James aliwahimiza wazalishaji hasa wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kuwa na uhakika wa soko.
Alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wajasiriamali ni kutozalisha bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo, ndiyo maana shirika hilo linatoa huduma hiyo kwao bure, kwani Serikali inatenga fedha kwa ajili yao kila mwaka.
Kwa mujibu wa James wametumia maonesho hayo kutoa elimu hiyo kwa wajasiriamali kwani mitaani kumekuwa na taarifa za upotoshaji kwamba ni gharama kuthibitisha ubora wa bidhaa.
"Sisi tunasema hakuna gharama, Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuthibitisha bidhaa zao. Wanachotakiwa ni wao kupitia SIDO na wakishapata barua ya utambulisho wanaileta kwetu na mchakato wa kuthibitisha bidhaa zao unaanza mara moja," alisema James.
Social Plugin