NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WANAHARAKATI wa Jinsia na Maendeleo wameshauri kuwekwa kwa sheria kali ili kudhibiti vijana na wanawake kujihusisha na matumizi ya vilevi kupindukia pamoja na kuongeza nguvu kwenye utoaji wa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na utumiaji wa vilevi kupit kiasi.
Ushauri huo umetolewa leo Juni 26, 2024 katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika kila Jumatano kwenye viwanja vya TGNP- Mtandao, Mabibo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Mwanaharakati Dorice Alchard amesema kwenye matumizi ya vilevi kupindukia waathirika wakubwa ni wanawake, vijana na watoto ambapo kwenye upande wa watoto wanashindwa kupata haki zao za msingi kama elimu na malezi bora kutokana na ulevi uliopo katika familia.
Amesema baba au mama akiwa ni mlevi wa kupindukia anasababisha shughuli za kijamii zisiendelee kufanyika kwani anakuwa hajiwezi kufanya jambo lolote la msingi ikiwemo utoaji wa mawazo mazuri ambayo yangeweza kusaidia kuleta faida.
"Ulevi wa kupindukia unaathari kubwa sana kwenye familia na hata kwenye jamii kuwa ujumla, mlevi hawezi kufanya jambo lolote la msingi, kazi zinasimama kutokana na ulevi wa mtu husika na muda mwingine kusababisha ugomvi kama tunavyoshuhudia mara nyingi kwenye jamii inayotuzunguka". Amesema
Kwa upande wake Mwanaharakati Rachel Mjema amesema matumizi ya vilevi yanachangia matukio mbalimbali ya kikatili kwenye jamii, kama vile wizi, matusi, ubakaji kutekeleza familia, migogoro ndani ya ndoa, ongezeko la watoto mtaani, afya ya akili pamoja na matukio mengine mengi ambayo kwa ujumla yanamuathiri kwa kiwango kikubwa mtoto wa kike.
Nae Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mabibo, Nasma Khamis amesema matumizi ya vilevi yanasababisha watoto kutokuhudhuria masomo darasani pamoja na kujihusisha na mapenzi katika umri mdogo jambo ambalo linaweza kumplekea kukatisha ndoto zao za msingi.
Social Plugin