Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WATAKIWA KUJIFUNZA MIFUMO YA KISHERIA KUEPUKA MIGOGORO ISIYO YA LAZIMA





Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nchini Jumanne Sagini leo June 28,2024 ametembelea Kliniki ya Ushauri na elimu ya Sheria kwa Umma kwenye viwanja wa Mwalimu Nyerere(Nyerere Square) iliyozinduliwa hivi karibuni kujionea namna msaada wa kisheria unavyotolewa kwa wananchi ili kupunguza migogoro dhidi ya Serikali na kupata suluhu ya changamoto.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya utoaji ushauri wa kisheria na kuzungumza na wananchi waliokwenda kupata huduma za kisheria kwenye Kliniki hiyo, ameeleza kuwa kati ya changamoto zinazowakabili wananchi kwa kiasi kikubwa, suala la migogoro ya ardhi ndilo limeshika kasi.

Amesema ili kutafsiri ndoto za Rais Samia,wanasheria wanapaswa kuimarisha utawala bora wa Sheria nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira bora ya utoaji huduma kwa jamii na kuepukana na vitendo via rushwa vinavyoweza kuchochea migogoro ya ardhi.

Akiongea na Wataalam hao wa sheria amesema wananchi wanahitaji zaidi msaada wa uelewa wa sheria na mamlaka ya Serikali na Mahakama kwa kuwa wanaiamini Serikali yao hivyo ni vema wakaelimishwa ili wapate uelewa.

"Tumebaini kuwa licha ya jitihada za Wizara ya Ardhi kuanzisha kliniki Maalum za utatuzi wa Migogoro ya Ardhi na utoaji wa elimu, hadi sasa imeonekana bado kuna tatizo kubwa, watu wanadhulumiwa haki yao ,Wizara ya Ardhi ina jukumu kubwa la kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi na kuepusha kuendelea kushamiri kwa migogoro hiyo, "amesisitiza
Mbali na hayo ameishukuru ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuunga Mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha utoaji wa haki kwa wananchi baada ya kubainika kuwa wengi hawakuwa wanapata kwa wakati na wakati mwingine walinyimwa kabisa stahiki zao.

Amesema zaidi ya watu 50 wamepatiwa msaada wa Kisheria kwenye Kliniki hiyo na kupatiwa msaada kulingana na kero zao huku malalamiko ya migogoro ya ardhi yakishika kasi jambo lililopekelea Naibu waziri huyo kutoa rai kwa viongozi mbalimbali wa Serikali kuendelea kuisaidia Serikali kupunguza Migogoro kabla haijafika ngazi ya Wizara na kuelezea dhamira ya Wizara ya katiba na Sheria kufika Mikoa yote kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Kwa upande wake Odessa Horombe ambaye ni Mwakilishi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Mkoa wa dodoma ameeleza kuwa moja kikwazo kinachokwamisha kufanikiwa kwenye eneo la uelewa wa kisheria ni wananchi wengi kutojua kusoma wala kuandika .

Kutokana na hayo ametoa wito kwa wananchi kuwa na ari ya kujifunza uelewa wa mifumo ya kisheria ili waweze kuzifahamu kwa ufasaha sheria zinazotumika kutatua migogoro.

Horombe pia amesema kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia wananchi wamekuwa sehemu ya mabadiliko kwa kuelewa namna ya kutafuta suluhu ya malalamiko yao na kueleza kuwa kero za wananchi ni wajibu wao hivyo wataendelea kuzitatua kupitia Kliniki ambayo ilizinduliwa June 26,2024 Jijini Dodoma huku ikitarajiwa kuhitimishwa Julai 3,2014 .





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com