Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SEKTA YA MADINI YAJIPAMBANUA KWA WANANCHI

Imeelezwa kuwa Sekta ya Madini imeanza kujipambanua kipindi cha miaka ya karibuni baada ya kufanyika marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 na kuonyesha kuvutia Watanzania wengi kuliko ilivyokuwa kabla ya kufanyika mabadiliko hayo.

Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na watu wanaotembelea mabanda ya Wizara ya Madini na Taasisi zake yaliyopo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya  Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam. 

Moja kati ya Watu hao, Gregory Kumbuka Mkazi wa Ilala Jijini Dar es Salaam amesema kuwa yeye binafsi alidhani kuwa shughuli za Sekta ya Madini zinahusu wawekezaji wa nje kwa kuwa zinahitaji mitaji mikubwa, lakini kupitia vyombo mbalimbali vya habari ameongeza uelewa wake kuhusu sekta ya madini.

Amesema kuwa, mbali na vyombo hivyo vya habari, pia, kupitia maelezo aliyoyapata kwenye mabanda ya Wizara ya Madini na Taasisi zake, imemsadia kumwongezea uelewa zaidi kuhusu sekta hiyo na kwamba kwa maeneo anapofanyia shughuli zake anafikiria kuwekeza kwenye Madini ya Ujenzi kama mchanga na kokoto.

Kwa upande wake, Salma Fahadi mkazi wa Morogoro Mjini amesema kuwa ameweza kujifunza kuhusu sekta ya madini kupitia vyanzo tofauti ikiwemo vyombo vya habari kwani hapo awali alikuwa hafahamu kuwa mchanga na kokoto ni madini na ili mtu aweze kuchimba kwa tija anahitaji kufuata utaratibu maalum ikiwemo kuomba leseni.

Ameongeza kuwa, kupitia elimu aliyopata pia kupitia wataalam wa Wizara na Taasisi zake waliopo katika Maonesho hayo, anafikiria kutumia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini kwa mtu mmoja mmoja lakini pia kupitia vikundi.

Wizara ya Madini na Taasisi zake zinashiriki Maonesho hayo kwa pamoja kwa lengo la kutoa elimu kuhusu Mnyororo mzima wa shughuli za uchimbaji wa madini kwa manufaa ya kiuchumi na maendeleo endelevu kwa ujumla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com