Kampuni ya uzalishaji wa umeme jua ambayo inamilikiwa na Mhe. Stephen Masele ambaye ni Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Shinyanga Mjini na Makamu wa Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika imesaini mkataba wa ujenzi wa megawati 100 za umeme wa Solar ambao utaingizwa katika gridi ya taifa.
Hafla ya utiaji saini kati ya SSI ENERGY TANZANIA LTD na Mhandisi Alex Wu ambaye ni mkurugenzi mkazi wa kampuni ya kimataifa ya Sinohydro Corporation kutoka nchini China ambao ndiyo wakandarasi watakaojenga mradi huo imefanyika leo Julai 26,2024 katika ofisi za SSI ENERGY TANZANIA jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Masele Stephen amesema Mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya taifa na hususani Kanda ya Ziwa ambayo imekuwa na matatizo ya upungufu wa umeme.
"Hakika leo historia imeandikwa kwa kampuni ya kizalendo kufanya uwekezaji mkubwa wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 300 za Kitanzania.
Kampuni yangu imekuwa katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa megawati 10mw ambao unagharimu zaidi ya bilioni 30 za kitanzania hapo Kahama katika vijiji vya Chapulwa na Mondo ambapo mradi wetu utakamilika mwezi Machi 2025, hivyo tunayofuraha kubwa leo kusaini kandarasi ya ujenzi wa hatua ya pili ya mradi mkubwa katika historia ya nchi ya ujenzi wa megawati 100mw", amesema Mhe. Masele.
"Eneo la Kahama ni moja ya maeneo ya Kimkakati kwa kuwa baada ya kufungwa kwa Mgodi wa Buzwagi eneo hilo limegeuzwa kuwa eneo la uwekezaji na kuvutia miradi mbali mbali ya kimkakati, mfano Mgodi wa Tembo(Kabanga Nickel) unatarajia kujenga rifainali ya kuchakata nickel ambapo watajitaji matumizi makubwa ya umeme ikikadiriwa kufika megawati 75mw, vile vile Kahama ni sehemu muhimu ya kibiashara katika ukanda wa ziwa victoria.
SSI ENERGY inakuwa kampuni ya kwanza ya kizalendo kufanya uwekezaji mkubwa hapa nchini katika sekta ya umeme jadidifu (renewable energy)", ameongeza Masele.
Social Plugin