*Asisitiza ushirikiano, amani, upendo kufikia matarajio ya Sekta
*MAHIMBALI amweleza mlango uko wazi kutoa ushauri kwa Sekta
*STAMICO Yasema uongozi wake ulikuwa wa Manufaa Makubwa kwa Shirika
Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema ataendeleza pale alipoishia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Kheri Mahimbali kutekeleza majukumu na kusimamia masuala yote yanayohusu Sekta ili kuhakikisha malengo tarajiwa ya Taifa kupitia Sekta ya Madini yanafikiwa.
Ameyasema hayo Julai 9, 2024 katika hafla yupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Katibu Mkuu baada ya kuteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kushika wadhifa huo wa kuisimamia Wizara ya Madini.
Ili kufikia matarajio hayo, Mhandisi Samamba amewataka Watumishi wote wa Wizara na Taasisi zake kufanya kazi kama timu moja huku akihimiza upendo, ushirikiano, amani na kuoneana huruma kuhakikisha malengo ya Wizara ya kukusanya Shilingi Trilioni Moja katika Mwaka wa Fedha 2024/25, utekelezaji wa vipaumbele vyake, utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 na utekelezaji wa Vision 2030: Madini ni Maisha& Utajiri yanafikiwa.
Mhandisi Sambamba ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza aliyekuwa Katibu Mkuu Kheri Mahimbali kutokana na usimamizi na uongozi wake uliopelekea maendeleo na mafanikio kwenye Sekta ya Madini ikiwemo ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ya kiasi cha Shilingi Bilioni 753 katika Mwaka wa Fedha 2024/25 na kueleza kwamba, ni mafanikio ambayo akiwa Katibu Mtendaji wa Tume wa Madini hayakuwahi kufikiwa.
‘’Tunayo majukumu mbele yetu kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la taifa kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 au kufika mapema kabla ya mwaka huo. Katibu Mkuu Mahimbali ametuacha na asilimia 9.1 ni mafanikio makubwa sana, tuna asilimia 0.9 iliyobaki tuendelee kujiamini tukamilishe. Lakini ili kufikia hapa, kila mmoja kwenye eneo lake awasimamie watu wake vizuri,’’ amesisitiza Mhandisi Samamba.
Kwa upande wake, Mahimbali akizungumza katika kikao hicho, amemweleza Mhandisi Samamba kuwa anayo timu nzuri ya kumsaidia kutekeleza majukumu yake kikamilifu kutokana na ubobezi walionao katika masuala yanayohusu Sekta ya Madini na kutumia nafasi hiyo kumweleza yuko tayari kusaidia pindi Wizara itakapohitaji ushauri kutoka kwake kwa maendeleo ya Sekta ya Madini.
Mahimbali ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kumteua kusimamia majukumu mbalimbali ya Serikali kuanzia alipokuwa Naibu Katibu Wizara ya Nishati hadi kufikia hatua ya kuwa Katibu Mkuu Madini na kumpongeza kwa kumteua Samamba kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini kutokana na historia yake kwenye Sekta ya Madini.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo ameeleza kuwa mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika Sekta ya Madini yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya wizara, taasisi na wadau wa Sekta ya Madini na kutumia fursa hiyo kumpongeza Mahimbali kwa miongozo na usimamizi aliokuwa akiutoa uliopelekea kufikiwa kwa mafanikio hayo.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amesema uongozi wa Mahimbali kwa Shirika hilo ulikuwa wa manufaa makubwa kutokana na maono ya kutaka taasisi hiyo kujiendesha kibiashara kufikia viwango vya kampuni kubwa duniani na kueleza kwamba, katika mwaka huu wa fedha shirika hilo litaanza kulipa mishahara ya wafanyakazi bila kutegemea fedha kutoka Serikali na kumwomba pia kufungua milango kwa taasisi hiyo pindi itakapohitaji ushauri kutoka kwake.
‘’ Wengi wasiojua, uongozi wa Mahimbali kwa STAMICO ulikuwa wa manufaa makubwa sana, tulikaa mkao wa Shirika tuwe kama Barrick na GGM, focus yake ilikuwa shirika liwe la kibiashara,’’ amesema Dkt. Mwasse.
Social Plugin