Mkuu wa wilaya ya Mvomero Judith Nguli (kulia) akipokea madawati 60 kutoka kwa kamanda wa uhifadhi Sylivester Mushy
Na Christina Cosmas, Morogoro
MAMLAKA ya usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imekabidhi madawati 60 yenye thamani ya shilingi Milioni 5 kwa shule ya msingi Changarawe iliyopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Akikabidhi madawati hayo kwa niaba ya Kamishna wa uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda Kamanda wa uhifadhi kutoka kanda maalum ya Dar es salaam Sylivester Mushy alisema Mamlaka itaendelea kushirikiana na jamii katika miradi ya maendeleo na kukabiliana na tatizo la wanayamapri wakali a waharibifu kulingana na bajeti itakavyokuwa inapatikana.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli alisema wananchi wananufaika sana na uwepo wa TAWA kutokana na ufadhili wao katika miradi ya maendeleo na pia kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu wilayani humo.
Nguli alisemaTAWA imeleta neema kwao kwa kuwakabidhi madawati 60 ili kusaidia shule ya msingi Changalawe iliyopo kata ya Mzumbe Wilayani humo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa madawati kwenye shule hiyo uliokuwa unasababisha wanafunzi kukaa chini.
Alisema ushirikiano unaooneshwa na TAWA kwa jamii inayowazunguka ni mfano wa kuigwa ambao unapaswa kuzingatiwa katika kuimarisha mahusiano kwa jamii na kuweka usimamizi mzuri wa masuala ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na misitu nchini.
“Nichukue nafasi hii kuishukuru TAWA kwa uwepo wake katika wilaya ya Mvomero kama wadau wa uhifadhi, pia tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia kwa mipango yake ya kuiwezesha TAWA kifedha kwa sababu imetusaidia sisi wananchi wa Mvomero kupata huduma ya madawati na vile vile kukabiliana na tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu” alisema Nguli.
Hivyo Mkuu huyo wa wilaya aliiomba TAWA kutochoka kutoa ushirikiano na kuhakikisha ulinzi shirikishi wa masuala ya wanyamapori unasimamiwa kwa pamoja na jamii na hivyo kuweka msimamo katika suala zima la usimamizi wa wanyamapori na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Social Plugin