Na Hadija Bagasha Pangani,
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala amezindua mpango wa vitambulisho vya msamaha wa matibabu kwa wazee Wilayani humo akitahadharisha wahudumu wa afya kuhakikisha kila mwenye kitambulisho anahudumiwa bila kupuuzwa.
Kilakala ametoa kauli hiyo wakati akizindua mpango rasmi wa kugawa vitambulisho vya msamaha kwa wazee katika zahanati ya Kigurusimba iliyopo kata ya Masaika Wilayani humo.
Aidha Kilakala amemuagiza mganga mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha vitambulisho hivyo haviwi mapambo na badala yake vitumike kuwasaidia wazee hao pale ambapo sitahitaji matibabu kwenye kituo chochote cha afya ndani ya Wilaya hiyo.
"Kitambulisho ni jambo moja na matibabu ni jambo la pili niwaombe wataalamu wangu Mganga mkuu wa Wilaya wazee hawa wasiwe na vitambulisho hivi vikawa kama mapambo vikawasaidie kweli wanapokwenda kwenye vituo vya afya au zahanati wanapokwenda kwenye hospitali yetu ya Wilaya, "
"Nitake wazee hawa wapate matibabu bure kama ambavyo Rais wetu alivyoelekeza wasinyanyaswe wala wasiwekwe watu wa mwisho kwasababu tu wanavitambulisho wanatibiwa bure, "alisisitiza Kilakala.
"Nitoe maelekezo haya na DMO uyashushe kwa wataalamu wako Zahanati zote na Vituo vyote vya afya kwamba wazee hawa wakionyesha vitambulisho watibiwe haraka sana na si tu kutibiwa bali baada ya vipimo kuonyesha wana matatizo gani wapatiwe dawa sababu hivyo vitambulisho vya msamaha pia dawa ipo ndani yake, "alisema Kilakala huku akiliinua jina la Rais Dkt. Samia.
Social Plugin