Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi leo alasiri anatarajiwa kuzungumza na wananchi wa Lindi kwenye mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika Uwanja wa Mpilipili, Mjini Lindi.
Balozi Nchimbi na msafara wake, atapokelewa rasmi asubuhi ya leo katika Ofisi za CCM za Mkoa huo, ambapo atafanya kikao na Kamati ya siasa na baadaye mkutano wa ndani wa makundi mbalimbali.
Lengo la ziara hiyo ni; Kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020, kuhuisha uhai wa chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhakiki Taarifa zao na kujiandikisha katika Daftari la Wapiga kura, kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Novemba mwaka huu.
Katika ziara hii Dk Nchimbi kabla ya kuingia mkoani Lindi, amemaliza ziara ya siku mbili mkoani Mtwara, ambapo ameambatana na Katibu wa NEC-Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndg. Amosi Makalla, Katibu wa NEC-Organaizesheni Ndg. Issa Ussi Haji (Gavu) pamoja na Katibu wa NEC- Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Rabia Abdallah Hamid.