Banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) limeendelea kuwa kivutio kwa Wananchi mbalimbali wanaotembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Wananchi wengi wanaotembelea Banda hili wamefurahishwa na huduma zinazotolewa hasa elimu ya kuhusu huduma za Kibandari na shughuli mbalimbali za utekelezaji huku wakitoa pongezi kwa TPA kwa kuwa na mpango bora wa kutoa elimu kwa umma na hasa matumizi ya mifano ya meli na mashine mbalimbali za kutolea huduma Bandarini.
Banda hili limekuwa kivutio sio kwa Wananchi tu bali hata kwa Viongozi mbalimbali wa Serikali wanaotembelea ambapo wametoa pongezi nyingi kwa Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa TPA kwa utendaji kazi wenye ufanisi na kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali Nchini.
Aidha Viongozi hao wamepongeza ushirikiano wa TPA na Wabia wake wa Kibiashara katika kutoa huduma Bandarini na kuhimiza ushirikiano zaidi kutoka watumiaji wengine wa Bandari ili kuongeza tija, ufanisi na mchango wa sekta ya Bandari katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.
Kivutio kingine katika Banda la TPA ni uwepo wa Wabia kampuni ya DP World iliyoanza kutoa huduma Bandari ya Dar es Salaam mwezi Machi mwaka huu, pamoja na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) ambao kwa pamoja wamekuwa wakielezea mipango na mikakati yao ya kuongeza viwango vya ubora wa utoaji huduma katika Bandari.
Maonesho haya yanayowakutanisha Wafanyabiashara, Wakulima, Wafugaji na Wajasiriamali kutoka ndani na nje ya Nchi, yameanza tarehe 28 Juni, 2024 na kufunguliwa rasmi tarehe 3 Julai, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na yanatarajia kufungwa tarehe 13 Julai, 2024
Social Plugin