Na Hadija Bagasha Tanga,
Mjumbe wa kamati ya siasa wilaya ya Mkinga Twaha Mwakioja amewataka vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo kuwa chawa wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuisemea miradi inayotekelezwa na serikali badala ya kuwa chawa wa mtu.
Mwakioja ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye baraza kuu la umoja wa vijana Wilaya ya Mkinga lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
"Vijana mnatakiwa muwe Chawa wa CCM Kwa maana mkisemee chama chetu na serikali yetu Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta miradi mingi kwenye wilaya yetu, tuna mradi wa Maji wa bilioni 35 ambao unatoa maji kutoka Tanga mjini Hadi Horohoro haya ndio mambo ambayo tunapaswa kuyasemea kama vijana, "alisisitiza Mwakioja.
Aidha jambo lingine alilosisitiza kwa vijana hao ni kuwaasa wasitumike vibaya badala yake wahakikishe wanakuwa sehemu ys kuchagua viongozi ambao watasaidia Mkinga kupiga hatua na si kuchagua viongozi wanaojali maslahi yao wenyewe.
"Wilaya yetu bado ipo Nyuma Sana katika mambo mengi ya kimaendeleo lazima tuchague watu ambao watatusaidia kuchochea maendeleo yetu, "alisema.
"Ndugu wajumbe wa baraza tunajua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, mbele yetu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa vijana msibaki nyuma katika nafasi hizi, "alisema na kuongeza
"Nawasihi vijana wale wenye sifa wakachukue fomu, Ili na wao wawe sehemu ya Viongozi wenye maamuzi, uongozi wa kitongoji, Kijiji una mamlaka kubwa katika nchi yetu kwavile nyie ndiyo mnaokaa na wananchi hivyo badala ya kulalamika nyie ndiyo mtaondoa changamoto zilizopo katika maeneo yenu, "alisisitiza Mwakioja. .
"Twendeni tukashiriki uchaguzi huu vijana wenzangu tukijua fika tunataka chama chetu cha CCM wilaya ya Mkinga tushinde Vitongoji na Vijiji vyote vilivyopo katika wilaya yetu, "alibainisha.
Mgeni Rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Erick Farahan ambaye ni Mjumbe wa mkutano mkuu wa Mkoa amesema vijana ni hazina kubwa ya chama hicho hivyo wasiishie kulalamika badala yake fursa zinapotokea wajitokeze na washiriki.
"Mnapaswa kujiona kwamba na nyinyi vijana mna sifa ya kushiriki nafasi mbalimbali ikiwemo za uongozi msijiweke nyuma Taifa linawategemea hakikisheni kupitia nafasi mlizokuwepo mnakwenda kuwa mabalozi wazuri wa kazi kubwa zinazotekelezwa na serikali yetu, "alisisitiza Erick.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa vijana Wilaya ya Mkinga Mwanaisha Rashid amewaasa vijana kuacha matumizi mabaya ya mitandao ikiwa ni pamoja na kuwapuuzia wale wote wanaokisemea vibaya chama hicho.
"Niwaombe vijana mshiriki kikamilifu katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji tusisubiri nafasi zimetangazwa ndio tukachukue fomu tuanze mapema kufanya maandalizi ya uchaguzi kwa kuendelea kuwahamasisha vijana wenzetu kwenda kujisajili kwenye daftari la wapiga kura, "alisema
"Jumuiya ya umoja wa vijana tuna kazi kubwa sana kwasababu tuna wimbi kubwa sana la vijana ambao hawapo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ukizingatia daftari lile kinaandikishwa na kuhuishwa kila baada ya miaka mitano ina maana kuna vijana wakati ule daftari linaandikishwa hawakuwa na umri sahihi wa kupiga kura, "alisema
Stamil Dendego Katibu wa ccm Wilaya ya Mkinga amewapongeza vijana wilayani humo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhamasisha mambo mbalimbali na kuwataka vijana hao wasitumike vibaya kwakuwa wapo baadhi ya viongozi wanatumia vibaya nembo ya vijana kufanya mambo yao.
Social Plugin