Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI ZANZIBAR WAJIONEA MAAJABU YA SHIRIKA LA KIVULINI, YASINI AVIMBA NA MBINU YA "SASA"


Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Abeida Rashid Abdallah amepongeza mchango wa Shirika la KIVULINI katika kutoa elimu ya kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Ametoa pongezi hizo Alhamis Julai 04, 2024 akiwa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kwenye ziara ya kimafunzo ya kujifunza mbinu za kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ya mbinu ya SASA iliyoonyesha mafanikio katika kampeni za shirika la Kivulini.

"Zanzibar tunatekeleza mpango wa kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wasichana na wanawake, tumekuja kujifunza mbinu hii ya SASA ili nasi ikatusaidie kutekeleza mpango huo" alisema Abdallah huku pia akimpongeza Mkurugenzi wa shirika la Kivulini, Yassin Ally kwa jitihada kubwa anazofanya kuelimisha jamii kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally alisema mbinu ya SASA (Start, Awareness, Support & Action) imesaidia jamii kutonyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa wasichana na wanawake ambao sasa wanashiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi pamoja na wenza wao huku matukio ya mimba na ndoa kwa wanafunzi wa kike yakipungua.

"Mbinu hii inashirikisha makundi mbalimbali ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa kuhusu masuala ya ukatili na anachukua jukumu la kuwaelimisha wenzake kukataa ukatili ambapo sisi tumekuwa na jukumu la kuwajengea uwezo" alisema Ally.


Baadhi ya wakazi wa Kata ya Sukuma wilayani Magu walikiri kuwa baada ya kupatiwa elimu, hivi sasa watoto wa kike wanapata fursa ya kupata elimu tofauti na awali pamoja na kutumia vyema mapato yatokanayo na shughuli za kilimo ikiwemo kujenga nyumba bora na kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abeida Rashid Abdallah wamefanya ziara ya kimafunzo ya siku tatu kuanzia Julai 03,2024 katika shirika la Kivulini ambalo limekuwa likitekeleza miradi ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita na Kigoma.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibari, Abeida Rashid Abdallah (katikati) akipokea taarifa ya utekelezaji mpango wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kutoka kwa Katibu Tawala Wilaya ya Magu, Jubilate Lauwo (kulia).
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Abeida Rashid Abdallah akizungumza na wakazi wa Kata ya Sukuma wilayani Magu baada kufika katika Kata hiyo akiwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara yake ili kujifunza mbinu ya SASA inayotumika kutoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana KIVULINI, Yassin Ally akieleza namna mbinu ya SASA ilivyosaidia kutoa elimu wilayani Magu na kusaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Wanaharakati wa kijitolea ngazi ya jamii kupitia kikundi chao cha mashabiki wa Simba wakieleza namna wanavyohamasisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Kata ya Sukuma wilayani Magu.
Msemaji wa mashabiki wa Yanga akieleza namba kikundi chao kilivyosaidia jamii kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Magu.
Akina mama wakitoa elimu kwa njia ya nyimbo.
Viongozi mbalimbali kutoka Zanzibari wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibari, Abeida Rashid Abdallah wamefanya ziara katika shirika la KIVULINI mkoani Mwanza kujifunza mbinu za kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na wasichana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com