MSEMAJI MKUU WA SERIKALI AWATAKA MAAFISA HABARI MWANZA KUWA WABUNIFU UHABARISHAJI UMMA


Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Thobias Makoba amewataka Maafisa Habari wa serikali Mkoani Mwanza kubuni habari mpya za kimkakati zenye kuitangaza miradi ya maendeleo ya serikali badala ya kusubiri matukio.

Bwana Makoba ameyasema hayo leo tarehe 19, Julai 2024 wakati alipokua akizungumza na Maafisa Mawasiliano kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, Taasisi, Mashirika na Makampuni  mbalimbali ya serikali Mkoa wa Mwanza katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Bwana Makoba amesema anatamani kuona Maafisa hao wakiwa wabunifu zaidi katika kuhakikisha wanauhabarisha umma kwa namna ambayo sio ya kutegemea habari kutoka kwa viongozi tu bali  watumie mbinu mbalimbali ili kuonesha utofauti wa utendaji wa sasa na siku za nyuma.

"Na hapa Mwanza ninajua kuna miradi mbalimbali ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya SGR hivyo tusisubiri ijitokeze  dosari ukimbilie kutoa taarifa ya ufafanuzi , ni wakati sasa wa kubadili  namna ya utoaji wa taarifa zetu". Amesisitiza Makoba.

Aidha, amesema umekua ni utaratibu wake kukutana na Maafisa Mawasiliano kila mahali aendapo lengo likiwa ni kujitambulisha lakini pia kusikiliza na kuchukua maoni, mawazo na mapendekezo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha utendaji kazi.

"Kuwa msemaji mkuu sio kwamba unajua kila kitu, tunategemeana katika kuhabarisha kwani serikali ni moja, " amefafanua Makoba.

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amesema Mkoa wa Mwanza ni Mkoa wa kimkakati kwa kuwa ndio lango kuu kwa kanda ya ziwa na ndio kitovu cha uchumi hivyo Maafisa Habari wanategemewa kwenye uhabarishaji na serikali inawapa ushirikiano mzuri.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (RS Mwanza) Bw. Paulo Zahoro amesema hali ya uhabarishaji kwa Mkoa wa Mwanza ni nzuri hata kufikia hatua ya kushinda nafasi ya pili na kupata Kikombe na Cheti cha Ushindi kutoka kwa Waziri wa Habari Mhe. Nape Nnauye kwenye Kongamano la Habari lililofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Juni mwaka huu.

Maafisa Mawasiliano nao wamemshukuru Msemaji Mkuu wa Serikali kwa kutambua umuhimu wao ambapo wamemuahidi kutimiza wajibu wao kwa kuhabarisha jamii juu ya mambo mbalimbali yanayotekelezwa na serikali.



 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post