WAZIRI UMMY MWALIMU APIGA MARUFUKU HOSPITALI KUMTOZA MWANANCHI POSHO YA MUUGUZI NA DEREVA KATIKA AMBULANCE


Na Hadija Bagasha Tanga, 

Waziri wa afya Ummy Mwalimu amepiga marufuku hospitali zote Nchini kumtoza mwananchi posho ya muuguzi na dereva wanaomsindikiza mgonjwa katika gari la kubebea wagonjwa ( Ambulance) na badala yake ameagiza hospitali husika ndio ibebe gharama hizo ili kumpunguzia mwananchi mzigo mkubwa huku mwananchi akitakiwa kuchangia mafuta peke yake. 


Pia Waziri Ummy ameagiza Waganga wakuu wa Mikoa kote Nchini kufanya mapitio ya gharama za wananchi kuchangia huduma za gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance)  ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi. 

Waziri Ummy amepiga marufuku hiyo wakati akikabidhi gari la kubebea wagonjwa katika hospotali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo ikiwa ni moja ya magari ya kubebea wagonjwa 727 yamenunuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwajili ya kusambazwa katika hospitali na Halmashauri mbalimbali nchini zoezi lililoanza mwezi novemba mwaka jana. 

Waziri Ummy amesema kuwa gharama za kumsafirisha mgonjwa kwenda kwenye hospitali ya rufaa zinakuwa kubwa  kutokana na kwamba posho ya dereva na ya muuguzi anabebeshwa mgonjwa wakati garama hizo zinapaswa kubebwa na hospitali. 

"Moja nalipiga marufuku mnataka wananchi wachangie posho ya muuguzi hapana kutoa posho ya muuguzi ni jukumu la hospitali sio jukumu la mgonjwa mwananchi achangie mafuta tu posho ya muuguzi na dereva ni jukumu la hospitali wakati mwingine gharama zinakuwa kubwa kwasababu tunamtaka mwananchi achangie posho yamuuguzi na dereva hapana hapana serikali tuchangie posho ya muuguzi na dereva mwananchi agharamie mafuta tu na mgonjwa ana haki ya kusindikizwa na muuguzi ndio utaratibu mgojnwa ambaye amepewa rufaa anabebwa na Ambulance ni lazima kuwepo mtaalamu wa afya, "alisema Waziri Ummy. 

"Mganga Mkuu wa Mkoa uko hapa na waganga wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania bara kila mtu afanye mapitio ya gharama za Ambulance na tukubaliane gharama ambazo ndio husika na kama imetokea kuna wagonjwa wawili wanashea gharama basi na ile inatakiwa kufanywa, "alisema Ummy. 

"Tunanunua haya magari kwa gharama kubwa sana inatuumiza kuona mwezi mmoja au siki tatu gari imeanguka kuna noja tuliigawa Iringa ndani ya siku 10 tu gari imeshaanguka kuna jambo kama serikali tunapaswa kulifanya kwamba madereva wa magari haya kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu za usalama barabarani, "alisistiza Waziri Ummy. 

"Mkoa wa Tanga umepata Ambulance 15 katika majimbo yote 12 kila jimbo limepata Ambulance 1 tusijisifu tu kwamba tumeleta magari 15 tunataka magari haya yatunzwe magari ya kubeba wagonjwa yatunzwe yafanyiwe matengenezo ili yaweze kukaa kwa muda mrefu kwasababu serikali inatumia fedha nyingi sana kuyanunua mfano hii gari ya leo tumetumia milioni 100 kuinunua, "alisisitiza Waziri Ummy. 

Hivyo Waziri Ummy ameagiza kutengwa kwa fedha kwajili ya matuzo na matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa kwakuwa ni lazima magari hayo yafanyiwe service ya mara kwa mara. 

Wakati huo huo Waziri Ummy amesema serikali kupitia wizara ya afya inaendelea kuhakikisha hospitali za rufaa za Mikoa Nchini zinakuwa na madaktari bingwa ili  mambo mengi yamalizikie kwenye Mkoa badala ya watu kupelekwa mbali zaidi. 

 Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wq Tanga Dkt. Imani Clemence amesema Ambulance iliyokabidhiwa leo imetimiza idadi ya Ambulance 15 kwa Mkoa mzima ambapo majimbo 12 yote yamepata. 

"Naomba kwa niaba ya Mkoa nikuahidi kwamba tutazitumia gari hizi kama ilivyoelekezwa,  tutazitunza,  na kuzifuatilia kila zinapokuwa zinafanya safari zake na kuhalikisha zinakuwa salama na kutoa zile zinazostahili" amesema. 

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani Bombo Dkt. Frank Shega amesema gari hiyo ya wagonjwa itaendelea kuboresha huduma za afya kwenye hospitali hiyo. 

"Nikuhakikishie mheshimiwa Waziri gari hii uliyotukabidhi leo tutaitunza kwa uwezo wetu wote tukiamini jitihada mheshimiwa Rais anazozifanya mpaka tumeweza kupata Ambulance hii itakwenda kuwahudumia wananchi wetu  kwa weledi zaidi, "alisema Dkt Shega. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post