ZANZIBAR
KAMATI ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa imezitaka taasisi zinazohusika na uwezeshaji wananchi kiuchumi kuweka mkakati wa kuungana kufanya kazi kwa pamoja ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokwaza ufikiaji wa haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake.
Wito huo umetolewa kufuatia ziara ya wajumbe wa kamati yenye lengo la kufuatilia utekelezaji wa Programu hiyo Zanzibar kubaini kuwepo kwa baadhi ya changamoto zinazowakwaza wanawake kupata haki na usawa wa kiuchumi.
Makamo mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mgeni Hassan alieleza licha ya wananchi hasa wanawake kuonesha utayari wa kujishughulisha na shughuli za kiuchumi hasa kilimo cha mwani lakini wanakabiliwa na vikwazo vingi vinavyowakatisha tamaa zaidi.
Alibainisha kutokana na changamoto hizo kugusa sekta mbalimbali ni muhimu taasisi husika kama Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Uchumi wa Buluu na nyingine zote kuweka mashirikiano ya kwenda kwa pamoja kutatua changamoto hizo ili lengo la haki na usawa wa kiuchumi lifikiwe.
"Kuwe na mashirikiano ya kitaasisi kwa kufika chini ngazi ya halmashauri huko, hii itatusaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha katika masuala mbalimbali kwenye kujenga kizazi chenye usawa wa kiuchumi," alieleza Mhe. Mgeni.
Aliongeza, “huko akinamama wengi tumeona wana shida nyingi za bei, kibiashara na mazingira magumu hasa wakulima wa mwani lakini ukiwaona wana moyo na wanahitaji sana kufanya shughuli hizo,” alieleza Mhe Mgeni.
Kwa upande wake Dkt. Monica Mhoja, mjumbe wa kamati hiyo alishauri serikali na wadau kuweka kipaumbele cha kutoa elimu kwa wanawake kutambua haki zao na kuchukua hatua sitahiki pale zinapokandamizwa.
"Tuweke mkakati wa kutoa elimu ya utambuzi wa masuala ya kisheria kwa wanawake katika kila eneo ili waweze kutambua haki zao na namna gani wanapaswa kufanya ili kupata haki hizo,” alieleza Dr. Mhoja.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Najma Hussein Abdallah, alishauri taasisi za uwezeshaji wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya utafiti ili kubaini mahitaji ya wananchi na kutafuta mbinu sahihi za kusaidia kutatua changamoto hizo.
Alieleza, " tunatakiwa kufanya utafiti wa kina kutambua wakulima wote wa mwani walipo ili kutusaidia kujua namna gani tunaweza kuwafikia wote na kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili. Hatuwezi kwenda kama bado hatujaitambua hali halisi ya wakulima.”
Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu, Cpt. Hamad Bakar Hamad alipogeza kamati hiyo kubaini uwepo wa changamoto hizo na kuahidi kushirikiana na taasisi zote ili kuhakikisha sekta ya uchumi wa buluu na uwezeshaji wananchi kiuchumi inakuza uchumi wa wananchi hasa wanawake ambao ndio wadau wakubwa wa kilimo cha mwani Zanzibar.
Alikiri licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na taasisi mbalimbali kukuza uwezeshaji wananchi kuchumi kwenye sekta tofauti, changamoto kubwa iliyopo ni kukosekana mashirikiano ya kisekta na kupelekea kila taasisi kufanya kivyake.
Alisema, "Cordination ya kusimamia uchumi wa buluu haitaishia hapa Zanzibar tu, tutakaa na wenzetu Bara kwani wakulima wa mwani wanaoathirika sio wa Zanzibar tu hata wa bara kukitokea changamoto kwenye bahari nao wanaathirika, hivyo lazima tukae pamoja tuone namna gani tunaweza kushirikiana kutatua changamoto hizo.”
Kamati hiyo ya kitaifa inaendelea na ziara Zanzibar inayolenga kufuatilia utekelezaji wa Programu hiyo na jitihada za kukuza haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake nchini.
Social Plugin