Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VISWASWADU KUTUMIKA KUBORESHA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

 

Wapiga kura waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wataweza kutumia simu zao ndogo za mkononi (vitochi au viswaswadu) kuanzisha mchakato wa kuboresha au kuhamisha taarifa zao. 

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani leo tarehe 18 Julai, 2024, uamuzi huo wa Tume umetokana na maoni ya wadau wa uchaguzi. 

“Tume imefanyia kazi maoni na ushauri huo (wa wadau) na kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 watu wote wenye simu za kawaida (maarufu kama kitochi au kiswaswadu) na watahitaji kuboresha au kuhamisha taarifa zao, watapata huduma hiyo kwa kupiga USSD Code *152*00# na kubonyeza namba 9 kisha kuendelea na hatua zingine kama itakavyokuwa inaelekezwa kwenye simu husika,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mpiga kura anayetumia njia hii atapokea namba maalum (token) kupitia simu yake kisha atalazimika kwenda na namba hizo kwenye kituo anachotarajia kutumia kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kukamilisha mchakato na kupewa kadi mpya.

Katika hatua nyingine, Tume imetoa taarifa kwa umma kuhusu kuanza rasmi kwa kituo cha huduma kwa mpiga kura (Call Centre) kinachoanza kutoa huduma kuanzia leo Alhamis tarehe 18 Julai, 2024. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Bw. Kailima, huduma hiyo ni ya bure na itatolewa kwa saa 14 kila siku kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku.

“Kupitia kituo hiki wananchi watapata fursa ya kupiga simu bila malipo kupitia namba 0800112100 na kupata majibu au ufafanuzi wa maswali au jambo lolote linalohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, wananchi wote mnakaribishwa kutumia huduma hii kwa kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com