Chifu Edward Makwaia.
Na Marco Maduhu,KISHAPU
TAMASHA la Utamaduni Sanjo ya Busiya, ambalo hufanyika kila Mwaka Kijiji cha Negezi Kata ya Ukenyenge Wilayani Kishapu, katika familia ya Chifu Makwaia huwa linakutanisha maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yakiwamo ya kiutamaduni.
Tamasha hilo hufanyika kila mwaka kuelekea Siku kuu ya Sabasaba, ambapo ndani ya wiki nzima hufanyika sherehe za kitamaduni, pamoja na kufanya Ibada ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka na kupata mavuno ya mazao, na pia kuombea mbegu za mazao katika msimu ujao wa kilimo.
Chifu Edward Makwaia akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 6,2024 katika kuelekea kuhitimishwa kwa Tamasha hilo hapo kesho Julai 7, ambalo litahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kimila kutoka ndani na nje ya nchi, Serikali pamoja na Wananchi,amesema Tamasha la mwaka huu litakuwa la aina yake na pia Serikali wamewaunga mkono.
Amesema Tamasha hilo la Utamaduni Sanjo ya Busiya,lengo lake ni kuwakutanisha Watu pamoja na kuenzi Tamaduni zao, huku wageni kutoka nje ya nchi watajifunza pia Tamaduni za kabila la Wasukuma ikiwamo na kufanya Utalii wa Mali Kale.
Kaburi la Mtemi Makwaia.
“Tamasha hili la Utamaduni Sanjo ya Busiya, hua linakutanisha Watu zaidi ya Elfu 40 na hujifunza mambo mbalimbali ya kuenzi Utamaduni wetu, kupendana na kudumisha Amani,”amesema Chifu Makwaia.
Aidha, amesema Tamasha hilo hutumika pia kusukuma ajenda za Serikali kwa kufikisha ujumbe kwa wananchi, na kwamba mwaka huu kuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo utatolewa ujumbe kuhamasisha wananchi wajitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo, na kuchagua viongozi sahihi wenye kuwaletea maendeleo.
Katika hatua nyingine Chifu Makwaia,ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia “Chifu Hangaya” kwamba katika Utawala wake amekuwa Rais wa tofauti kwa kuwatambua Machifu, na hata kuwaunga Mkono na kuwashirikisha pia katika shughuli mbalimbali za kiserikali.
“Rais wetu Samia amekuwa tofauti sana na Tawala zingine zilizopita, ni kiongozi ambaye hana majivuno na hata kututambua sisi Machifu, na Tamasha la Mwaka huu la Utamaduni Sanjo ya Busiya,Serikali imetuunga Mkono pia tofauti na miaka yote,”amesema Chifu Makwaia.
DC Mkude.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, amesema Matamasha hayo ya Jadi yanaisaidia Serikali katika mambo mbalimbali ikiwamo kuenzi Tamaduni zao, kuleta ushirikiano katika Jamii na hata kufanya kazi kwa pamoja kikiwamo kilimo kupitia vikundi.
Ametaja faida nyingine ni kusukuma ajenda mbalimbali za Serikali, na kutolea mfano mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kwamba kupitia Tamasha hilo wananchi watafikishiwa ujumbe huo, pamoja na kupewa taarifa za miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa na Serikali ikiwamo ya kimkakati.
Naye Chifu wa Wakamba Augustus Muli kutoka Kenya, amesema wamekuja kuona Tamasha hilo la Utamaduni la Sanjo ya Busiya, na wamefurahi kuja kusherehekea kama jamii, na waafrika ni jamii moja, na kwamba Wasukuma na Wakamba wana chanzo kimoja na walioana na kuzaliana na kueleza kuwa ndiyo maana Wasukuma wana Majina mengi ya Wakamba.
Naye Mjukuu wa Chifu Mwakaia Nicolaus Luhende, ametoa wito kwa wananchi, kwamba kesho wajitokeze kwa wingi kwenye hitimisho la Tamasha hilo, ili wajifunze mambo mbalimbali ya kitamaduni.
Wakamba kutoka Kenya wakipiga picha ya pamoja, ambapo Tamasha la Sanjo ya Busiya litahitimishwa kesho Siku ya Saba 7 Negezi wilayani Kishapu
Social Plugin