Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Kahama Mhandisi Joseph Kumburu akitoa agizo kwa uongozi wa mgodi wa Nyikoboko akiwataka kupanga maeneo pamoja na usafi wa mazingira
Meneja wa Mgodi wa Nyikoboko Charles Izengo akielezea kuhusu usafi wa mazingira ya mgodi huo
Na Neema Israel - Malunde 1 blog Kahama
Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu waliopo mgodi wa Nyikoboko Halmashauri ya Msalala Mkoa Shinyanga wamelalamikia ukosefu wa huduma ya choo katika mgodi huo ambao umeanzishwa wiki tatu zilizopita.
Mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu, Maganga Emanuel ameeleza kuwa hali ya mgodi huo ni mbaya kwani hakuna choo wanajisaidia popote hali inayohatarisha afya zao.
"Hali ya mgodi ni mbaya maana hakuna choo tunajisaidia mahali popote ambapo nitaona hapa nitajisitiri hili hii inatishia afya zetu kwa sababu huwezi kufanya kazi kama hauna afya nzuri", amesema Maganga.
Naye Mfanyabiashara wa chakula katika mgodi huo, Rehema Hassan ameuomba uongozi wa mgodi kuwajengea choo ili waweze kuendelea kufanya biashara zao maana yakitokea magonjwa ya mlipuko watafukuzwa.
Kwa upande wa ulinzi na usalama wa mgodi huo, Anold Benedicto amesema wamejipanga kuhakikisha watu wanaoingia katika mgodi huo wanakuwa salama.
Pia Katibu wa Kamati ya ulinzi wa mgodi huo amesema wamejipanga kukabiliana dhidi ya ukatili kwa wanawake katika eneo la mgodi kwani wanawake wanaonewa kwa kudhulumiwa na kubakwa.
Aidha meneja wa mgodi huo Charles Izengo ameeleza kuwa tayari choo kimeshaanza kuchimbwa hivyo amewasihi wachimbaji kuendelea kutumia vyoo vya nyumba za wageni pindi wanaposubiri vyoo vya mgodi vikamilike.
Hata hivyo Afisa madini mkazi Mkoa wa kimadini Kahama Mhandisi Joseph Kumburu amewataka uongozi wa mgodi kupanga maeneo ili kuweka mazingira salama pia kushughulikia suala la vyoo haraka.
"Tumewaambia mpange haya maeneo maduara yawe sehemu yake, muweke maeneo ya makazi na maeneo ya chakula maana ndio mazingira yenyewe pia kuwe na maeneo ya vyoo wasimamizi kuanzia kesho vyoo vianze kutengenezwa, hiyo ndio afya yenyewe", amesema Mhandisi Kumburu.
Mgodi huo mpaka sasa una wachimbaji wadogo zaidi ya 3,000.
Mfanyabiashara wa chakula katika mgodi huo, Rehema Hassan akielezea hofu aliyonayo juu ukosefu wa vyoo endapo magonjwa ya mlipuko yakitokea watashindwa kufanya biashara
Katibu kamati ya ulinzi wa mgodi Sikujua Edward akizungumzia hali ya usalama
Social Plugin