Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

IMARISHENI USIMAMIZI WA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI- NDUNGURU




Na Angela Msimbira, MWANZA

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Adolf Ndunguru amewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi chini kuhakikisha wanaimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kuongeza ubunifu katika utatuzi wa changamoto za ujifunzaji kwa wanafunzi.

Ndunguru ametoa maagizo hayo leo Julai 11,2024 jijini Mwanza wakati akifunga mafunzo kwa walimu wakuu na maafisa mazingira kuhusu miongozo ya ujenzi wa miundombinu ya shule, usalama wa mazingira na jamii na taratibu za ununuzi wa umma.

Amesema Serikali imeanza kutekeleza. itaala ya elimu iliyoboreshwa inayosisitiza utolewaji wa elimu itakayomwezesha mwanafunzi kupata ujuzi ili aweze kujitegemea na kuliletea Taifa maendeleo hivyo ni wajibu wa kila walimu kuhakikisha anatimiza majukumu yake kikamilifu.
Pia amewaelekeza walimu wakuu wote nchini kuhakikisha wanaweka mazingira wezeshi yatakayowasaidia walimu kushiriki kikamilifu Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) katika ngazi ya shule na vituo vya walimu ili kuboresha ufundishaji.

“Serikali imedhamiria kuboresha ufundishaji kupitia Mpango wa mafunzo endelevu kazini, hivyo nitumie fursa hii kuwaelekeza walimu wakuu wote nchini kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha walimu kushiriki kikamilifu katika MEWAKA na kuwapa usaidizi unaohitajika” amesema Ndunguru

Amesema kuwa uwepo wa mazingira salama na rafiki kunamuwezesha mwanafunzi kujifunza kwa ufasaha hivyo amewataka walimu hao kuweka mifumo na mikakati ya kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa aina yoyote.
Amewataka kuhakikisha klabu za wanafunzi zinahuishwa na wanafunzi kujengewa uwezo wa kujitambua, kujieleza, kujiamini na jamii ishirikishwe katika kuweka utaratibu wa kubaini na kushughulikia masuala ya ukatili, unyanyasaji na malalamiko.

Aidha, amewataka kuhakikisha wanasimamia ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya shule kwa wakati huku ujenzi huo ukiendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali ili kuweza kuleta manufaa kwa taifa na kutimiza vigezo vya kupata fedha,

Programu ya BOOST imekwishatoa jumla ya Sh bilioni 311.3 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu tangu mwaka 2022/23 ambapo awamu ya kwanza zilitolewa Sh bilioni 230 na awamu ya pili zimetolewa ya shilingi bilioni 81.2 kwenye shule za msingi 699 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 78, vyumba vya madarasa 1,625 matundu ya vyoo 3,635, nyumba za walimu 10 na ukarabati wa shule


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com