Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi (mbele) akiongoza kikao cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) kilichofanyika leo Jumatatu Julai 15, 2024 Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma.
KAMATI ya Usimamizi wa Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) imekutana kwa ajili ya kupitia taarifa za utekelezaji wa mradi huo.
Katika kikao hicho cha nne kilichofanyika leo Jumatatu Julai 15, 2024 kimeongozwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi ambapo amesema mradi huo utaongeza uwezo wa kitaasisi katika kuimarisha uzingatiaji wa sheria na mifumo ya utekelezaji.
“Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira umekabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa rasilimali watu na rasilimali fedha katika utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya rasilimali mazingira katika ngazi zote. Mradi huu umekuja na suluhisho la changamoto hizi” amesema Mitawi.
Wajumbe wa kikao hicho pia walipitia taarifa ya utekelezaji wa mradi kwa mwaka wa fedha 2023/24 pamoja na bajeti ya 2024/25, ambapo Mitawi amewahimiza kuusimamia vyema mradi katika utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira
Pia wajumbe wa kikao hicho walipata fursa ya kuipitia taarifa ya mpango wa matumizi kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2023 na kukamilika Juni 2024 kama ulivyowasilishwa na Mratibu wa Mradi Bw. Richard Masesa.
Itakumbukwa kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imefanya jitihada kadhaa za kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kuweka Sera ya Kitaifa ya Mazingira (1997) pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004).
Mradi wa EMA unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Swedish (SIDA) unakusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira na kuondoa vizuizi vya kisekta vilivyopo katika Wizara na mamlaka maalumu za kisheria na kuongeza wigo wa utendaji.
Mradi wa EMA unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika katika Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma leo Jumatatu Julai 15, 2024. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Immacuate Sware.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akifurahia jambo na Mwakilishi wa Ubalozi wa Sweden, Bw. Steven Mwakifwamba muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) kilichofanyika katika Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
(PICHA NA MPIGAPICHA WETU)
Social Plugin