Na Ferdinand Shayo ,Manyara .
Kampuni ya kuzalisha vinywaji changamshi yenye makao makuu yake Mjini Babati Mkoani Manyara ya Mati Super Brands Limited imesaini mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi pamoja na Kampuni ya Muziki ya Bongo Records inayoongozwa na Producer Maarufu PFunk Majani kwa lengo la kuwezesha Matamasha Mbali mbali ya Muziki wa Wasanii Wakongwe na kutangaza bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ikiwemo Tanzanite Royal Gin,Strong Dry Gin,Tanzanite Premium Vodka kupitia muziki.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mati Super Brands Limited David Mulokozi amesema kuwa mkataba huo unalenga kufanya kazi na wasanii wakongwe wa Bongo Fleva na kuwapa mashabiki burudani waliyoikosa kwa muda mrefu Pamoja na kuhakikisha wasanii hao wanaendeleza sanaa yao licha kuwa balozi wa bidhaa hizo.
Mulokozi amesema kuwa Matamasha Makubwa ya Bongo Fleva yatafanyika katika mikoa ya Dar Es salaam ,Arusha,Mbeya,Dodoma na Iringa kwa lengo la kutoa burudani kwa Watanzania na wapenzi wa bidhaa wanazozalisha.
“Nimefurahi sana kuona wasanii wetu wakiongozwa na Juma Nature,Matonya ,Ferouz,Daz Baba,Domokaya na Wengine wengi nina hakika mkataba huu utakua na manufaa kwa pande zote mbili Bongo Recods na Kampuni yetu ya Mati Super Brands Limited” Anaeleza David Mulokozi.
Mkurugenzi wa Bongo Records ambaye ni producer Mkongwe Pfunk Majani amesema kuwa wamejipanga kufanya matamasha Makubwa ndani na nje ya nchi ili kukonga nyoyo za mashabiki.
“Tumejipanga kurudisha Heshima ya Bongo Fleva tunaishukuru sana Kampuni ya Mati Super Brands Limited kwa kutoa udhamini huu unaowawezesha Wasanii kuwa mabalozi wa vinywaji wanavyozalisha” Alisema Pfunk.
Kwa Upande wao Wasanii wa Bongo Fleva akiwemo Juma Nature,Jay Mo na Linah wameishukuru kampuni hiyo kwa kuwajali na kuwaenzi Wasanii wakongwe huku wakiahidi kufanya makubwa.
Social Plugin