Naibu waziri wa Nishati Nchini Mheshimiwa Judith Kapinga ameanza ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani humo.
Ziara hiyo imeanza leo Julai 01, 2024 ndani ya halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama na kutarajia kutamatika ifikapo Julai 03, 2024 ndani ya manispaa ya Kahama.
Akizungumza kwa niaba ya
wananchi wa jimbo la Ushetu Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Emmanuel Cherehani
amesema Jimbo la Ushetu lina vitongoji 524 ambapo bado kuna baadhi ya maeneo
hawajafikiwa na huduma ya umeme hivyo kumuomba mkandarasi kuongeza kasi ya
utekelezaji.
“Jimbo la Ushetu lina kata
20 na Vitongoji 524 lakini bado kuna baadhi ya maeneo hawajafikiwa na umeme
nikuombe Mheshimiwa naibu waziri wa Nishati wananchi hawa wamesubiri kwa muda
mrefu lakini mpaka leo bado hawajasogezewa huduma ya umeme hali hii
inasababisha shughuri za maendeleo kukwama kwenye baadhi ya maeneo”, amesema
Chereheni.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo alipotembelea kijiji cha Sunga kata ya Uyogo halmashauri ya Ushetu Naibu waziri wa Nishati Nchini Mheshimiwa Judith Kapinga amemtaka mkandarasi anayetekeleza usambazaji wa umeme wilayani Kahama kupitia kampuni ya Tontan Project Technology Co. Ltd Jv Group Six International kueleza ni lini atamaliza utekelezaji wa mradi huo kwenye vijiji vyote ndani ya wilaya ya Kahama.
Akijibu
swali hilo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tontan Project Technology Co. Ltd
Jv Group Six International, John Zheng amesema ifikapo Julai
10 mwaka huu wanatarajia kukamilisha usambazaji wa umeme kwenye vijiji vyote
ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme.
Aidha Mheshimiwa Judith Kapinga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza miudombinu ya umeme ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kwa manufaa ya vizazi na vizazi lakini pia kujiunganishia umeme kwenye maeneo ambayo tayari yamekwishafikiwa na huduma hiyo.
Akizungumza
kwa niaba ya serikali ya mkoa kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Wakili Julius
Mtatiro ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga amesema serikali ya awamu ya
sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo usambazaji wa umeme maeneo ya
vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA.
Katika ziara hiyo ya kikazi ya Naibu waziri wa Nishati Nchini Mheshimiwa Judith Kapinga pia ametembelea katika Kijiji cha Nimbo kilichopo kata ya Chona pamoja na kijiji cha Nyawishi kata ya Chambo ndani ya halmashauri ya Ushetu.