Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KATIMBA AWATOA HOFU WANAFUNZI WALIOUNGULIWA NA DARASA UYUI


Na Angela Msimbira , UYUI

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Zainabu Katimba amewatoa hofu wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lolangulu iliyopo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora ambao walikumbwa na janga la moto kuwa serikali itasaidia katika urejeshaji wa miundombinu.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo leo Julai 25,2024 Katimba amesema baada ya kupokea taarifa ya tathmini ya uharibifu uliotokea wataangalia namna ya kusaidia katika urejeshaji wa miundombinu hiyo.

“Sisi kama Ofisi ya Rais-TAMISEMI na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba niwaambie tu tunatambua adha kubwa ambayo mnakutana nayo. Sasa miundombinu yetu ndiyo kama hivi imepata changamoto nataka niwahakikishie kwamba tunasubiri ripoti ya tathmini ya kina.

“Na sisi kama Ofisi ya Rais Tamisemia tutashirikiana nanyi kuona namna gani tunaweza kuwaunga mkono katika janga hili ambalo mmelipata la uharibifu wa miundombinu ya darasa ambalo imetokana na moto, hivyo ujio wangu utakuwa na faida.”

Aidha, Mhe. Katimba amewaomba wananchi kuendeleea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anapambana kuwaletea maendeleo wananchi.

"Ninashukuru kamati ya ulinzi na usalama na wazazi ambao mmesaidia kuzima moto na kuokoa mali za umma zisiendeleee kuteketea zaidi"

Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lolangulu, Justine Machage amesema katika tukio hilo hakuna mwanafunzi aliyepata madhara ya kujeruhiwa au kupoteza maisha na chanzo chake hakijabainika.

Amesema vifaa vilivyoteketea ni darasa lenye thamani ya Sh milioni 26, magororo 30 ya wanafunzi wa kidato cha pili na nne ya wavulana, ndoo za kuogea, sare za shule, vitabu, daftari, mabegi ya nguo na masanduku ya kutunzia vifaa vya wanafunzi (trunke).

Awali, Diwadi wa Kata ya Ilolangula Mohamedi Linso amesema baada ya taarifa za moto kuenea wananchi walikusanyika na kuunganisha nguvu za kudhibiti moto uliokuwa unazidi kwa kuvunja ukuta wa vyumba ili kuzie usiendee kwenye vyumba na magengo mengine.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Said Ntahondi amesema halimashauri imechukua hatua za dharura za kuhakikisha wanafunzi hao wanaendelea na kambi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com