Na Hamida Kamchalla, TANGA.
SERIKALI imewaomba wadau wa sekta ya anga nchini na nje ya nchi, kuwekeza kwa kuleta ndege kufuatia maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika kwenye viwanja vya ndege na kuongezeka kwa abiria.
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ametoa ombi hilo alipotembelea kujagua maendeleo ya uboreshaji wa uwanja wa ndege jijini Tanga ambapo amesema maboresho yanayoendelea kufanyika nchini ni makubwa hivyo wadau wanahitajika.
"Tunawaomba wenzetu sekta binafsi watusaidie kuja kuwekeza katika sekta hii, nunueni ndege za kutosha kwa sababu Air Tanzania peke yake haiwezi kununua ndege katika viwanja vyote vinavyoboreshwa nchini,
"Kuna maombi ya kuongeza ndege katika Mikoa ya Mbeya, Tabora, Songea, Rukwa na Mpanda, lakini pia Kuna maombi ya kuongeza ndege safari za Dodoma kwenda Mbeya, Mwanza na Kilimanjaro na pia bado kuna viwanja viwanja vingine ukarabati wake haujakamilika" amesema.
"Tukiagiza ndege kwenye Shirika hili hazitoshi, lakini wadau binafsi wakileta ndege za kutosha wataunga mkono juhudi za serikali na ndege zitakuwa zinatosha, mizigo itasafirishwa na aboria watasafiri, kipato kitaongezeka kwa nchi na ajira kitaongezeka" amesisitiza.
Naibu huyo amebainisha kwamba hiyo ni kwa uwekezaji wa ndani lakini pia ipo fursa kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza ndege katika uwanja wa Dar es salaam kwakuwa ndege za Mashirika mengine zinzotua kutoka Duniani kote.
Aidha Kihenzile amesema serikali ya awamu ya situ chini ya Rais. Dkt. Samia Sulluhu Hassan mbali na maboresho ya viwanja vya ndege pia imedhamiria kwa dhati kuboresha sekta nzima ya Uchukuzi ambapo zipo bandari pamoja na reli nchini.
Naye Meneja wa Kiwanja cha ndege Tanga Yusufu Sood amesema serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) Ina mpango wa kuboresha Kiwanja hicho na kuongeza barabara ya kuruka na kutuma ndege kutoka mita 1268 hadi 1800.
Mbali na hilo itaboresha pia jengo la aboria, usimikaji wa mfumo wa taa za kuongozea ndege, ujenzi wabuzio wa kuzunguuka kiwanja, ujenzi wa eneo la kuegesha magari na ujenzi wa kituo cha huduma za kuzima moto.
"Mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hiki utawezesha kutatua kero zilizopo sasa za uchakavu wa miundombinu hasa barabara ya kuruka na kutuma ndege, kuboresha mfumo wa taa za kuongozea ndege na nyinginezo,
"Ukamilishaji wa mradi huu pia utawezesha kuchochea na kuongeza shughuli mbalimbali za kitalii, kiuchumi na kibiashara ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ajira kwa wananchi na hivyo kupunguza umasikini kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga" amesisitiza.
Mbali na hilo Sood amefafanua kwamba pindi maboresho yatakapokamilika hata tatizo la wavamizi katika maeneo ya kiwanja hayatakuwepo lakini pia vijana watapata ajira kupitia ujenzi yuo.
Kaimu Meneja wa TANROADS, Yussuph Pogwa naye amesema mradi huo ni sehemu ya mradi mkubwa unaofanywa na serikali ukihusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja 11 Tanzania Bara.
Pogwa amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi uko kwenye hatua ya manunuzi na mkataba unatarajiwa kusainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Septemba mwaka huu.
"Benki ya Dunia ilishatoa ruhusa ya kufanya ya Mhandisi Mshauri na usimamizi pamoja na Mkandarasi wa ujenzi wa mradi na mchakato wa manunuzi ukiratibiwa na TANROADS, Makao makuu" amebainisha Pogwa.
Social Plugin