Na Mwandishi wetu _Malunde 1 blog
WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya habari Nape Nnauye, amesema kupitia mradi wa Tanzania Kidijitali,itajengwa minara 758 ya mawasiliano kwa nchi nzima, katika mkoa wa Shinyanga itajengwa minara 30 na kunufaisha wananchi 421,259.
Waziri Nape amesema yao leo Julai 19,2024 alipofanya ziara mkoani Shinyanga, kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya mawasiliano.
Amesema serikali ya Tanzania kupitia pia Benki ya Dunia imepata fedha Dola milioni 150 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidigital,ili kijenga minara ya mawasiliano 758 kwa nchi nzima, na kuboresha mawasiliano hasa maeneo ya vijijini, na kwamba Shinyanga inajengwa minara 30.
"Lengo la mradi huu Tanzania tusiachwe kwenye fursa za kidigitali,na hapa Shinyanga inajengwa minara 30 kwenye Kata 29,Vijiji 83 na wananchi 421,259 watanufaika na kupata mawasiliano,"amesema Waziri Nape.
"Utekelezaji wa mradi huu tunafanya kazi na mfuko wa mawasiliano kwa wote "UCSAF" lengo ni kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata mawasiliano,"ameongeza.
Aidha, ameiomba Serikali ya Mkoa wa Shinyanga kusimamia ujenzi wa minara hiyo,huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutafuta fedha na kujengwa minara 758 kwa wakati mmoja.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kutoka (UCSAF), Justina Mashiba, amesema katika minara 30 ambayo inajengwa Shinyanga tayari minara 9 imeshawashwa,na kwamba kati ya minara 758 ambayo inajengwa nchi nzima,minara 186 imewashwa na inatoa huduma,na kwamba katika ujenzi wa minara hiyo wanashirikiana na kampuni za simu za mkononi.
Mkurugenzi wa leseni na ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) John Daffa, amesema hali ya mawasiliano kwa Mkoa wa Shinyaga ni nzuri,na kwamba kuna jumla ya minara 257.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,ameipongeza Serikali kwa kuimarisha mawasiliano hadi maeneo ya vijijini na kutoa wito kwa wananchi wawe na matumizi sahihi ya mitandao na kuahidi kusimamia kikamilifu ujenzi wa minara hiyo pamoja na kuimarisha ulinzi.
Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya habari Nape Nnauye akiwasili mkoani Shinyanga kwaajili ya ziara hiyo.