Zaidi ya wakazi 200 wa mtaa wa Mlalakua kata ya Makongo, Wilaya ya Kinondoni wanaenda kunufaika na mradi wa uboreshaji Usafi wa Mazingira unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa gharama za shilingi Milioni 33.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa usafi wa mazingira DAWASA, Miriam Mgata ameeleza kuwa mradi unaenda kwa kasi kubwa na muitikio umekua mkubwa kwa wananchi wengi kujitokeza kuomba huduma.
"Mradi huu unahusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba za inchi 8 kwa umbali wa mita 660 na utanufaisha zaidi ya wakazi 200 wa eneo la Mlalakua na maeneo jirani" ameeleza Mhandisi Mgata.
Mwenyekiti wa mtaa wa Malalakua ndugu Suleimani Massare ameipongeza DAWASA kwakusikiliza changamoto yao na kuja kutekeleza mradi huu kwa haraka sana huku akiridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi.
"Tulipeleka ombi DAWASA tupatiwe mradi huu, baada ya kuona mtaa wetu unachangamoto ya majitaka kutiririka mtaani, niwapongeze kwa kusikiliza kero yetu na kuja haraka kutupatia mradi huu, tunaimani utakapokamilika tutaepukana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kwani Mazingira yetu yatakua safi na salama" ameeleza ndugu Massare.
Mradi huu ni Mahususi kumaliza changamoto za utiririshaji Majitaka katika mtaa wa Mlalakua ambao unakabiliwa na changamoto ya kina cha maji kuwa juu na kupelekea vyoo kujaa mara kwa mara.
Social Plugin