Naibu Waziri wa Nishati nchini Mheshimiwa Judith Kapinga amesema mradi wa uzalishaji wa nishati ya umeme wa Julius Nyerere unatarajia kuzalisha megawati mara mbili ya umeme uliopo sasa hapa nchini pindi utakapokamilika.
Waziri Kapinga amesema hayo leo Julai 03, 2024 wakati wa mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kidunyashi kata ya Isagehe manispaa ya Kahama ikiwa ni hitimisho la ziara yake ndani ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa
mkutano huo Mheshimiwa Kapinga amesema kukamilika kwa mradi wa uzalishaji umeme
wa Julius Nyerere utapunguza changamoto ya mgao na kukatika kwa
umeme kwenye maeneo mbalimbali.
"Serikali
inatekeleza miradi mingi sana kwenye sekta nishati ya umeme ambazo ni
uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, ndiyo maana iliamua kutenga takribani
shilingi Tilioni 6 kwaajili ya ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa Julius
Nyerere ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata umeme wa uhakika na pindi
utakapokamilika utaweza kuzalisha megawati za kutosha ambazo ni mara mbili ya
umeme tuliona kwa sasa", amesema Mheshimiwa Kapinga.
"Lakini pia ipo
miradi ya usambazaji na kutanua mtandao wa umeme kwenye vijiji mbalimbali
ambapo kupitia wakandarasi wanaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini REA
kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinafikiwa na huduma ya umeme, suala la
umeme kwenye serikali yetu ni kipaumbele chetu", ameongeza Mheshimiwa
Kapinga.
Awali akieleza hali ya
upatikanaji wa umeme kwenye kata ya Isagehe Diwani wa kata hiyo amesema mpaka
sasa kati ya vijiji 24 vijiji 8 ndiyo vimefikiwa na huduma ya umeme vitongoji 8
bado havijafikiwa na huduma hiyo hivyo wamemuomba mkandarasi kuongeza kasi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Wakili Julius Mtatiro ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga amewasihi wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi wake.