Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Naibu Waziri wa Nishati nchini Mheshimiwa Judith Kapinga amewahakikishia wananchi upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye maeneo yote ya vijiji na vitongoji vilivyopo halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ifikapo 2025.
Ameyasema hayo Julai
02, 2024 wakati wa ziara yake ya ukaguzi ndani ya halmashauri ya Msalala ikiwa
ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ndani ya wilaya ya Kahama.
Mheshimiwa Kapinga amesema
dhamira ya serikali ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha kila kijiji na
kitongoji kufikiwa na huduma ya umeme ifikapo 2025 kama inavyosema ilani ya
chama hicho na kuwaahidi wananchi kuwa ataendelea kusimamia utekelezaji wa
miradi ya usambazaji umeme ili kufanikisha dhamira ya serikali na kuwaondolea
changamoto wananchi.
“Tumekuja hapa kuhakikisha
changamoto za wakazi wa Msalala zinapatiwa ufumbuzi , mengi yamezungumzwa
ikiwemo mafanikio na changamoto, ni kweli yapo maeneo yenye uhitaji
mkubwa wa umeme hususani maeneo yenye kukua kwa kasi, kama serikali
tunaendelea kusambaza huduma ya umeme na kutoa kipaumbele kwenye maeneo yenye
uhitaji na niwatoe hofu nitahakikisha sehemu zote ambazo zimetajwa kuwa na
changamoto ya umeme hadi ifikapo 2025 maeneo yote yatakuwa yamefikiwa na
umeme”, amesema Mhe. Kapinga.
Awali akieleza hali ya
upatikanaji wa nishati ya umeme kwenye halmashauri hiyo mbunge wa jimbo la
Msalala Mheshimiwa Iddi Kassim amesema kulingana na kukuwa kwa kasi kwa
halmashauri hiyo kwenye maeneo mbalimbali inasababisha uhitaji mkubwa.
“Tunaishukuru serikali yetu kwa kutuletea umeme vijijini lakini bado kuna changamoto ya uhitaji, kati ya kata 18 za halmashauri hii zipo kata ambazo zinakuwa kwa kasi sana ikiwemo Kagongwa ambapo bado mtandao wa umeme ni mdogo ukilinganisha na uhitaji uliopo hivyo tunaiomba serikali yetu kupitia Naibu Waziri wa Nishati dada yangu Mheshimiwa Judith Kapinga tuongezee angalau ili wananchi hawa waweze kufanya kazi zao kwa uhuru bila kuhofia lolote",
"Lakini pia mimi kama Mbunge na mwakilishi
wa wananchi nitaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kuhakikisha fedha anazoleta katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo zinafanya kazi kama ilivyokusudiwa na serikali”, ameongeza Mheshimiwa
Iddi.
Akizungumza kwa niaba ya serikali ya mkoa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Wakili Julius Mtatiro ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo usambazaji wa umeme maeneo ya vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA na kuipongeza REA kwa kuendelea kusambaza umeme kwenye maeneo mbalimbali kupitia wakandarasi waliowaweka.
Social Plugin