Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANASHERIA MKUU APONGEZA USIMAMIZI WA SHERIA YA USALAMA NA AFYA KAZINI


Na Mwandishi Wetu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, ameupongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini.

Ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la OSHA katika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba) yanayoendelea katika Viwanjwa vya Saba Saba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Temeke Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Feleshi alipokelewa na mwenyeji wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, ambaye alimweleza jinsi Taasisi hiyo yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa inavyotekeleza majukumu yake ya msingi.

“Ili kutimiza wajibu wetu wa kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, tunaanza kwa kutambua maeneo ya kazi kwa kuyasajili na kisha kuweka utaratibu mzuri wa wataalam wetu kufika katika maeneo husika kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya na kushauri maboresho yanayohitajika,” ameeleza Mtendaji Mkuu.

Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA, ameeleza kuhusu mkakati unaotumika na OSHA kuyafikia maeneo yote ya kazi nchini ambapo amesema mifumo ya TEHAMA ndio nyenzo inayotumika kuyafikia maeneo ya kazi mengi kiurahisi.

“Tunatumia mfumo wetu wa kieletroniki wa usimamizi wa taarifa za maeneo ya kazi (Workplace Information Management System-WIMS) ambao unatuwezesha kuwasiliana na wadau wetu kwa njia rahisi na haraka ambapo kupitia mfumo huo wadau wetu wanaweza kupata huduma zetu mbali mbali ikiwemo kusajili sehemu za kazi wakiwa mahali popote, kuwasilisha taarifa za ajali, kujisajili kupata mafunzo na kuwasilisha taarifa za ajali zinazotokea mahali pa kazi,” amefafanua Bi. Mwenda.

Akimweleza Mwanasheria Mkuu changamoto ambazo Taasisi ya OSHA inakabiliana nazo, Bi. Mwenda amesema changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa wananchi pamoja na kasi kubwa ya ukuaji wa teknolojia ya uzalishaji katika maeneo ya kazi ambayo huzalisha vihatarishi vipya kila mara.

Hata hivyo, Bi. Mwenda ambaye ndiye Mkaguzi Mkuu wa maeneo ya kazi nchini amesema Taasisi yake inazichukulia changamoto tajwa kuwa fursa kwa kuongeza program za kuelimisha umma pamoja na kuwekeza katika kuongeza utaalam wa wakaguzi wake ambao wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya mara kwa mara ndani na nje ya nchi ili kuendana na teknolojia mpya.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi mbali mbali katika sehemu za kazi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com