Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili kesho Julai 4,2024 Wilayani Bahi Mkoani hapa ukitokea wilaya ya Dodoma Mjini ambapo utahusisha ukaguzi na uzinduzi wa miradi Saba ya maendeleo .
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma Gift Msuya amezungumza hayo leo Julai 3,2024 Wilayani hapo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kuupokea Mwenge Wilayani hapo.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Uzinduzi wa nyumba ya walimu,Daraja, Vifaa tiba kwenye hospitali ya Wilaya, Mfumo wa gesi ya kupikia kwenye shule ya watoto wenye mahitaji maalum, MajiMaji na miradi ya vijana ikiwa ni hitaji la kutoa asilimia 4 kwa makundi ya vijana, wanawake na makundi maalum.
Amesema Mwenge huo utamulika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
"Maandalizi ya kuupokea mwenge yapo katika hatua za mwisho,tayari tumeimarisha hali ya ulinzi na usalama, ni bahati kubwa kuupokea baada ya kukimbizwa kwenye wilaya zote za Dodoma na sasa unakuja kuhitimishwa hapa tayari kabisa kwa mapokezi ya kuelekea Singida," amesema
Amefafanua kuwa kupitia Mwenge huo wa Uhuru ambao ni tunu kwa Taifa, Wilaya hiyo inatarajia kukamilisha kupanda miti milioni 1.7 kupitia vitalu miti kwenye shule za Sekondari na Taasisi za Umma.
"Tunajipanga zaidi kuhakikisha ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwenye Wilaya yetu unaimarishwa na kwa kuanza tayari tumesitisha vibali vya misitu ili kulinda mazingira, hakuna anayethubutu kukata miti na ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake," amesema Mkuu huyo wa Wilaya ya Bahi.
Kuhusu uchaguzi ulioko mbioni wa Serikali za Mitaa , Msuya amesema watatumia ujio huo wa Mwenge kuelimishana namna bora ya kufuata na kuzingatia kanuni za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwachagua viongozi wenye maono na Tanzania.