UZALISHAJI wa nguruwe Tanzania umekuwa ukiongezeka kutokana na uboreshwaji wa miradi unaofanywa na wafugaji nchini ambao wamekuwa wakiboresha ili kuendana na soko lililopo kwasasa ambsalo limeonekana kukua.
Ameyasema hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Mifuko, Wizara ya Mifugo na uvuvi, Dk. Stanford Ndibalema wakati wa uzinduzi wa mbegu mpya za nguruwe pamoja na uhimilishaji wa nguruwe kwa njia ya mrija uliofanyika Julai 27,2024 Jijini Dar es Salaam.
Amesema uzinduzi wa mbegu hiyo mpya utasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa nguruwe nchini na kuweza kukuza soko.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Naberera CTK, Bi Bensolight Msaki amesema kuwa tatizo la mbegu bora za nguruwe Tanzania litapungua sana kutokana na uzalishaji wa mbegu hizi mpya na bora.
Aidha amesema mbegu hizo mpya zinatarajiwa kuinua hali ya maisha ya watanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukua haraka pamoja na kuzaa vibwagala (watoto) wengi na wenye afya.
Nae Mwakilishi kutoka Bodi ya Nyama Bw. Kassimu Mnangwa amewataka wafugaji wa nguruwe nchini kufuata taratibu za ufugaji ikiwa ni pamoja na kupata usajili kutoka Bodi ya Nyama, ambapo usajili unafanyika kupitia mfumo wa kielectroniki wa mimis.mifugo.go.tz.
Mbegu mpya za nguruwe zilizozinduliwa ni majike aina ya CG36 na madume aina ya P81 (Pietrain), P26 (Duroc) na P90 kutoka Kampuni ya Choice/Axiom Genetics, Ufaransa.
Uzinduzi huo wa mbegu mpya za nguruwe uliambatana na mafunzo juu ya ufugaji na uhimilishaji yaliyoendeshwa na wawezeshaji kutoka Ufaransa, Uganda na Tanzania.
Social Plugin