Na Mariam Kagenda - Kagera
Wakuu wa Mikoa nchini wameagizwa kufanya operesheni ya kukamata waganga wa tiba asili na tiba mbadala wasio na leseni ambao wanajihusisha na ramli chonganishi zinazochangia vitendo vya kikatili dhidi ya Watu wenye Ualbino.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi leo Julai 9, 2024 Mkoani Kagera wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya watu Wenye Ualbino iliyozinduliwa katika kata ya Kamachumu mkoani Kagera ambayo imeambatana na kauli mbiu isemayo “Mimi nipo ninapinga ukatili dhidi ya watu Wenye Ualbino”
Vile vile, Mhe. Ndejembi amewataka Wakuu hao wa Mikoa kuhakikisha wanafanya kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino katika Halmashauri zote na kuhakikisha kamati za watu wenye ulemavu zinaimarishwa katika maeneo yao kwani ni takwa la kisheria kupitia sheria namba 19 ya mwaka 2010 ya watu Wenye Ulemavu.
Mhe. Ndejembi Pia ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa Mabalozi wa ulinzi wa Mtu Mwenye Ualbino kwa kutoa elimu, kupinga ukatili na kutoa taarifa kwa viongzo pale wanaposikia ama kuona viashiria vya ukatili dhidi ya watu hao.
Uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni siku chache tangu mtoto Asimwe Novath mwenye umri wa miaka 2 na nusu mwenye Ualbino kuuwawa kisha mwili wake kutupwa kwenye Karavati
Awali akizungumza Mkuu wa Mkoa wa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa amesema ataendelea kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino vinakomeshwa Mkoani humo.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania Alfred Kapole ameishukuru serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia kundi la Watu Wenye Ualbino ikiwa ni pamoja na kuwasaidia vifaa kinga.
Social Plugin