Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye viwanja vya Ikulu kwa ajili ya kuzungumza na Machifu kutoka Mikoa mbalimbali nchini, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Julai, 2024.
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan(Chifu Hangaya) ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuharakisha kukamilisha mwongozo wa utambuzi wa Viongozi wa Kimila(Machifu)utakao saidia Taasisi hiyo kujiendesha kwa kufuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosimamia haki za binadami na kuhimiza misingi ya usawa.
Rais Samia amesema hayo leo Julai 20,2024 Ikulu ya Chamwino mkoani hapa, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa kimila pamoja na Machifu kutoka mikoa yote nchini ambapo amewapa Machifu hao majukumu ya kusimamia amani na utulivu katika jamii, kutatua migogoro midogo-midogo, kusimamia matumizi ya ardhi na rasilimali za asili, na kuwakilisha jamii zao katika masuala ya kisheria na kisiasa.
Amesema Machifu ni Taasisi ya kijamii hivyo inapaswa kujiendesha kwa kufuata Katiba itayowasaidia kujipambanua na kujiepusha na vitendo vya unyanyasaji nanukiukwaji wa haki za kibinadamu ambao hutokana na adhabu za Kimila.
"Simamieni Mila na desturi, lakini angalieni adhabu mnazotoa kwa watu wenu ziendane na haki na usawa wa kijinsia ili kulinda hadhi ya jamii, msikiuke sheria, sitafurahishwa kuona chifu anakamatwa na jeshi la polisi kwa kukiuka sheria , " amesema
Mbali na hayo amekemea vitendo vya utekaji na mauaji ya watoto yanayoendelea hivi sasa nchini na kueleza kuwa Serikali isitupiwe lawama bali jamii inapaswa kuwajibika ili kukomesha hali hiyo.
Amesema Machifu huwa na heshima katika jamii zao na wanaweza kutoa mwongozo kwa vijana na wanajamii wao kuhusu maadili na mila za kabila hivyo ni muhimu kukemea vitendo vya utekaji pamoja na mauji ya watoto wakiwemo watu wenye ualibino hivi sasa vimeibuka kwa wingi katika maeneo mengi ya nchi hali ambayo inapaswa kukemewa na kuchukuliwa hatua kali.
“Hivi sasa vitendo vya utekaji pamoja na mauaji ya watoto vimekuwa vikiripotiwa kila siku na namna vinavyoripotiwa serikali ndiyo inalaumiwa sana wakati kule yanakotokea mambo haya viongozi wa mitaa wapo lakini hata machifu wapo wamekaa kimya.
“Nawaombeni mwende mkayakemee mambo haya kwani yanatokea huko kwenye jamii zetu na yanachafua taswira ya taiafa letu lenye sifa nje leo hii watu wakisikia mtu katekwa ama mtoto kuuwawa siyo picha nzuri,
Mambo ya mauaji ya alibino yalishapotea kabisa lakini sasa yanarudi kwa kasi na ukiuliza watu wanadai ni uchaguzi lakini uongozi anatoa Mungu siyo kwa kuuwa mtu”amesema Samia
Pamoja na hayo amewaagiza Machifu hao kushughulikia utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji kwa haki huku akiwatupia lawama wafugaji kuwa mara nyingi ndio huwa chanzo kwa kuwaonea wakulima.
“Lakini pia mkatatue migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikisababisha mauji ya watu na kuleta uhasama miongoni mwa wanajamii na mara nyingi wakulima ndiyo wanaoonewa,
mimi mwenyewe kuna kipindi nilikuwa nalima mpunga kule Morogoro kuna wakati mpunga ulistawi hadi nikasema umaskii sasa basi lakini siku moja tuu mfugaji aliingiza mifugo yake ndani ya dakika kumi tuu hakuna kilichobaki na nilipompeleka polisi anajibu kwa dharau tuu eti ngombe kala majani siyo mpunga”amesema
Vile vile, alimwagiza waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumaro, kuharakisha mchakato wa uandaji wa mwongozo utakaotumika kuwatambua na kuwasimamia machifu kutekeleza majukumu yao.
“Nikutake Waziri Ndumbaro huu mwongozo mhalakishe ili tupate kitu ambacho kitawatambua na kuwasimamia Machifu vingovyo tukiacha kila mtu afanye anavyotaka tutarudi kule ambako kutakuwa na uvunjifu wa katiba”alisema
Katibu wa umoja wa machifu Aron Mkomangwa, alisema wanaishuru serikali kwa kuwatambua na kuwashirikisha katika matukio mbalimbali ya kitaifa.
Mkomangwa, alisema wataendelea kuisaidia serikali kulinda maadili na kuzingatia mila na desturi za mtanzania.
“Mweshimiwa Rais pamoja na mambomengine lakini bado tunakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa jengo la ofisi ya makao makuu”amesema
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumaro, alisema wizara yake iko katika hatua za mwisho kukamiilisha mwongozo ambao utasaidia kuwatambua machifu wote pamoja na kazi zao wanazofanya.
“Mwongozo huu ni utekelezaji wa maagizo yako mweshimiwa Rais ya kutaka kuwepo na utaratibu maalum ambao utakuwa unatumika kuwatambua machifu kuanzia ngazi za mkoa hadi kijiji”alisema Dk. Ndumaro
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machifu nchini Chifu Antonia Siza Sangalale ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama na kueleza kuwa wao kwa nafasi yao wataendelea kushirikiana nayo katika kuhamasisha utii wa maadili.
Mbali na hayo ameeleza kuwa wataendelea kuenzi mila na desturi za kitanzania zinazojali utu na kubainisha kuwa kuna mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo Serikali inazipiga Vita hivyo wao pia watatumia nafasi zao kuzikataa kwa manufaa ya watanzania na ustawi wa nchi.
"Wewe ni nyota ya asubuhi yenye matumaini, utendaji kazi wako umepitiliza na kujulikana hata nje ya mipaka ya Tanzania, tunajiamini kwa kuwa umetuheshimisha kidunia na tunakuahidi kukusaidia kuijenga Tanzania yenye maadili inayosimamia haki, " amesisitiza
Kuhusu vitendo vya uvunjifu wa maadili na ukatili unaofanyika kwenye jamii,Chifu huyo ameeleza kuwa wao pia hawafurahii kuona kuna watu wanafanya uovu kwa namna yoyote na hivyo kusisitiza kuwa wataendelea kuisaidia Serikali kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma.
"Kuna desturi nyingine tunajua Serikali haizitaki, naomba nieleze pia sisi pia hatuzitaki na tutapingana nazo kwa nguvu zote ili kuiweka jamii kuwa salama,na kuondokana na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, " amefafanua Chifu huyo.
Social Plugin