Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AWAONYA WAVAMIZI MAENEO YA HIFADHI




Na Happiness Shayo - Katavi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuacha kuvunja sheria kwa kuvamia maeneo ya hifadhi na badala yake kutunza mazingira hayo.

Kauli hiyo imekuja kutokana na maombi ya Mbunge wa Mlele, Mhe. Isack Kamwelwe aliyeomba kumegewa ardhi katika maeneo ya hifadhi ya mapori yaliyopo jimboni kwake.

Ameyasema hayo leo Julai 13,2024 alipokuwa akizungumza na wananchi katika Wilaya ya Mlele, Kata ya Inyonga Mkoani Katavi.
"Tunajua kuna uhaba wa Ardhi na kuna maeneo ya hifadhi mnayatamani lakini hayaendani na kuvunja sheria tukae tuzungumze tuangalie namna ya kuyamega na si kuvamia" amesisitiza Mhe. Rais Samia.

Awali, akitoa ufafanuzi kuhusu ombi la Mhe. Kamwelwe la kuongezewa hekta elfu 15 katika Pori la Akiba Inyonga,Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea maombi hayo na inaendelea kufanya tathimini kuangalia uhitaji halisi na kuyawasilisha kwa mamlaka kwa hatua zaidi.

Amefafanua kuwa mwaka 2021 uamuzi wa Baraza la Mawaziri ulitoka ambapo hekta elfu kumi zilipunguzwa kwa ajili ya wananchi wa Kijiji cha Kamsisi.
Katika hatua nyingine Mhe. Kairuki ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Inyonga kuendelea kushirikiana na Serikali katika utunzaji wa mazingira, misitu na kuhakikisha hakuna uvamizi katika mapori.

Pia amewapongeza wananchi wa Katavi kwa kuwa na jitihada katika shughuli za ufugaji nyuki ambapo kuna wafugaji zaidi ya 2132 ambao wamewezesha kupatikana kwa zaidi ya shilingi bilioni 21.5.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com