RC MTWARA AIPONGEZA WIZARA YA FEDHA KWA KUTOA ELIMU YA FEDHA KWA WANANCHI


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Kenan Sawala, akizungumza na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara.

Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bahati Zeuze akizungumza na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara.

Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha - Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akitoa elimu ya fedha kwa wanavikundi na wajasiriamali katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu TTC - Kawaida Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Afisa Mkuu wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bi. Gladness Lema, akitoa elimu ya fedha kwa Wanavikundi na Wajasiriamali katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu TTC - Kawaida, Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonza, akitoa elimu ya fedha kwa Wanavikundi na Wajasiriamali katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu TTC - Kawaida, Manispaa ya Mtwara Mikindani


Afisa Msimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha- Wizara ya Fedha Bw. Jackson Mshumba, akitoa elimu ya fedha kwa Wanavikundi na Wajasiriamali katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu TTC - Kawaida, Manispaa ya Mtwara Mikindani

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Kenan Sawala,(katikati), Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Bahati Zeuze (watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha, walipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa elimu ya fedha kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa Mtwara, (watatu kulia) ni Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha - Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha)


Na. Chedaiwe Msuya, WF, Mtwara


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, ameipongeza Wizara ya Fedha kufuatia mpango wake unaolenga kuwapa wananchi uelewa wa masuala ya Fedha ikiwemo Usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji akiba uwekezaji, kinga za kibima na Mikopo iliyo salama kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wataalamu wa masuala ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi shiriki, waliomtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kutambulisha mafunzo hayo yatakayoendeshwa katika Wilaya zote za mkoa wa Mtwara.

"Naipongeza sana Wizara ya Fedha ikishirikiana na Taasisi nyingine zikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima, Benki Kuu, Masoko ya Mitaji na Dhamana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kwa kufika katika mkoa wetu kutoa elimu ya matumizi sahihi ya fedha itakayowasaidia wananchi kutumia fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo" Alisema Kanali Sawala.

"Nimeambiwa pia kuwa wananchi watapata elimu inayohusu masuala ya mikopo, nitumie pia nafasi hii kuendelea kuwashauri wananchi wanaohitaji mikopo kwenda kukopa kwenye Taasisi rasmi zilizosajiliwa kisheria kwa ajili ya usalama wa fedha zao” alisisitiza Kanali Sawala

Aidha, aliwaasa watoa Huduma Ndogo za Fedha Mkoani Mtwara na kwingineko kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019, na kuonya kuwa watakaotoa huduma hizo bila kufuata sheria watawajibishwa kwa mujibu wa sheria tajwa.

Kwa upande wake Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi, kutokana na wengi wao kuwa na matumizi yasiyo sahihi pale wanapopata fedha.

"Programu hii inalenga kuwafikia wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali, ili pamoja na mambo mengine wafahamu maeneo rasmi ya kupata huduma za fedha namna ya kuzisimamia fedha zao pamoja na kujiwekea utaratibu wa kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya kupata faida endelevu. amesema Kimaro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post