Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC SENYAMULE ANADI FURSA ZA SGR KWA WANANCHI WA DODOMA




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Macho na masikio ya Watanzania yakiwa yameelekezwa kwenye uzinduzi wa Reli ya kisasa ya mwendokasi unaitarajiwa kufanyika Agosti Mosi mwaka huu Jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassani, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka wananchi mkoani hapa kuitumia fursa hiyo kujiinua kiuchumi.

Akizungumza leo Julai 30 ,2024 Mkonze jijini hapa mara baada ya kukagua eneo hilo ameeleza kuwa hatua hiyo ya uzindua (SGR)inakuja wakati ambao tayari safari zake za majaribio zilianza Julai 25 kutoka Dar Es Salaam hadi Dodoma.

Amezitaja baadhi ya fursa zitakazotokana na Reli hiyo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za biashara kutokana na uwepo wa usafiri rahisi na wa haraka utakaochangia katika kuimarisha biashara na uwekezaji.

"Wafanyabiashara watakuwa na uwezo wa kufikisha bidhaa zao kwa wakati, na miji mingine itakuwa na fursa za biashara na ushirikiano na Dodoma,kuvutia wawekezaji kwa ujumla Reli ya mwendo kasi itafanya Dodoma kuwa kivutio zaidi kwa wawekezaji ambapo hali hii itachangia ukuaji wa viwanda, hoteli, na miradi mingine ya kibiashara,"amesema.

Sambamba na fursa hizo Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma amesema uwepo wa SGR utaongeza ajira mpya katika maeneo mbalimbali ambapo hali hii itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuboresha maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

Hali kadhalika amesema itasaidia Kuboresha miundombinu ya usafiri kwa kupunguza msongamano wa magari barabarani, kuboresha usalama, na kupunguza muda wa safari, hivyo kupunguza gharama za usafiri ikiwa ni pamoja na Kukuza utalii.

"Reli itavutia watalii kwa urahisi wa kufika Dodoma na maeneo mengine,hii itasaidia kukuza sekta ya utalii na kuongeza mapato kutokana na shughuli za utalii,kuimarika kwa huduma za kijamii,urahisi wa usafiri utawasaidia wananchi kufikia huduma muhimu kama vile afya na elimu kwa urahisi zaidi, hasa katika maeneo ya vijijini pamoja na Uendelezaji wa maeneo mapya, "amefafanua

Senyamule ametumia nafasi hiyo kuwataka Maofisa Usafirishaji(Bodaboda) watakaofanya usafirishaji wa abiria kwenye eneo hilo kufanya kazi kwa uaminifu na kueleza kuwa hali hiyo itawajengea uaminifu kwa wajeta wao na kuwasiaida kujiinua kiuchumi .

"Ni jukumu letu sote kulinda, kudumisha, na kutumia reli hii kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,mkiwa waaminifu mtafanya kazi yenu iaminike kwa jamii,tuwajulishe wengine kuhusu manufaa ya reli hii , na tuwe na umoja katika kuhakikisha kuwa Dodoma inakuwa mfano wa maendeleo na ustawi, "amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com