TANROADS DAR ES SALAAM YASAIDIA VITU VYA MILIONI 2 KWA WAHITAJI WA KITUO CHA MAMA THERESA MBURAHATI



Na Mwandishi Wetu

Watumishi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam jana wametoa msaada wa mahitaji muhimu kwa binadamu katika kituo cha Furaha na Amani cha Mtakatifu Thereza cha Mburahati jijini Dar es Salaam.

Akiongoza watumishi hao Meneja wa Mkoa huo, Mhandisi John Mkumbo amesema mahitaji hayo ya vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 2,030,000/= yamewasilishwa ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika kila mwaka nchini.
“Tunashukuru umetutembeleza kila mahali wanapoishi watoto wa umri mbalimbali, wazee wasiojiwe na watoto wenye changamoto ya kimwili, tumejionea mazingira yalivyo na hata uhitaji ninaamini kuna siku Mungu atatuongoza tutakuja tena kutoa mahitaji yanayostahili,” amesema Mha. Mkumbo.

Naye Mhasibu Mwandamizi wa TANROADS Dar es Salaam, Bi. Neema Mtengula amesema mbali na kuwa ni wajenzi wa barabara ili zipitike vizuri lakini pia wamekuwa wakitoa misaada kwa jamii zenye uhitaji katika vituo vya kulea wazee na watoto.

“Kwanza nakupongeza sana Sista kwa kazi ya utume unayofanya ya kuwalea watoto ni nadra sana kwa mama ambaye hana mtoto akaweza kumlea mtoto mwingine mwenye changamoto kwa mapenzi makubwa, nakupongeza sana kwa moyo wa upendo ambao Mungu ameuweka ndani yako,” amesema Bi. Mtengule.

Kwa upande wake Sista, M. Gonzalo M,C amewashukuru wafanyakazi hao wa TANROADS kwa majitoleo yao kwa ajili ya kituo hicho, amewaomba wasiwachoke na wafike mara kwa mara kuwasaidia maana bado wanauhitaji wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto na wazee wanaolelewa hapo.

Sista amesema kuwa wanawapata watoto wa kuanzia umri wa sifuri hadi miaka miatatu kutoka kwenye ofisi za Ustawi wa jamii wakiwa wengine wametelekezwa na wazazi wao hawajulikani, na wengine wanachangamoto za ulemavu wa viungo.


“Ninashukuru sana kwa moyo wenu mkuu mmeweza kutembelea nyumba yetu ya wahitaji mmejionea wenyewe wapo watoto wadogo sana jumla tuna watoto 34, wazee wasiojiweza 42 na watoto wenye changamoto mbalimbali za viungo wapo 22 bado tunahitaji misaada kutoka sehemu mbalimbali maana tuna watoto wadogo sana na wazee wengi hawajiwezi,” amesisitiza Sista Gonzalo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post