Na Mwandishi Wetu, Dar
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Thomas Bwana ametoa Wito kwa Wadau wa Kilimo, Wajasiriamali na wafanyabiashara kutumia matokeo ya Utafiti ili kunufaika kibishara na Uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa Kilimo.
Dkt. Bwana ametoa Wito huo , Julai 03, 2024 katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Kueleza hilo, Dkt. Bwana amesema Teknolojia za uongezaji thamani katika Mazao mbalimbali yanayofanyiwa Utafiti katika vituo vya TARI vinafungua fursa kwa wajasiriamali kujiongezea kipato pasina ulazima wa kujishughulisha na Kilimo.
Mfano wa hilo Dkt. Bwana anataja Teknolojia ya utengenezaji wa mvinyo kwa kutumia bibo la Korosho pamoja na mvinyo wa Zabibu ambazo ni Teknolojia zinapatikana katika vituo vya TARI.
Pia uzalishaji na uuzaji wa Mbegu bora za Mazao mbalimbali ikiwemo Mbegu bora za Mihogo ambazo Watafiti wamewajengea uwezo wa uzalishaji Mbegu hizo wajasiriamali wauzaji wa Mbegu bora za Mihogo zisizoshambuliwa na magonjwa ya batobato na Michirizi kahawia na wao wanaziuza kwa Wakulima katika maeneo mbalimbali ni miongoni mwa fursa za kibiashara anazotaja kuwepo katika Kilimo.
Kuendana na Kaulimbiu ya maonesho haya ya 48, Tanzania: Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji Dkt. Bwana amesema kama TARI wanaendelea kutafiti Teknolojia zaidi kulingana na uhitaji unaokuwepo wakilenga kuongeza tija ya mavuno kwa Mkulima na kutimiza malengo ya ajenda 10/30 ambayo ni Kilimo Biashara.
Danford John- Mkulima wa Mkonge Mkoani Tanga, alitembelea Banda la TARI katika Maonesho hayo, anaeleza kufurahishwa na upatikanaji wa Mbegu bora za Mkonge kutoka kituo cha TARI Mlingano ambapo anasema awali kabla hajaanza kutumia Mbegu bora ilikuwa ni kama anafanya Kilimo cha kubahatisha.
Social Plugin