Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh Anna Athanas Paul
Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dkt Mzuri Issa
ZANZIBAR
Naibu Msajili wa vyama vya siasa Mohammed Ali Ahmed amesema sheria na kanuni za maadili ya vyama vya siasa zinaendelea kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kuweka usawa wa kijinsia pamoja na kukuza uwajibikaji na kuzuia unyanyasaji dhidi ya wanawake ili waweza kushiriki kikamilifu katika siasa na demokrasia nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Msajili wa vyama vya siasa, Afisa sheria Mwandamizi kutoka ofisi hiyo Abdulrazak Ali kwenye mkutano wa tathmini iliyoangalia vikwazo vinavyowakwaza wanawake katika kugombea na kushiriki masuala ya kisiasa uliofanyika ukumbi wa ZURA Maisara mjini Unguja, ambao uliowashirikisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za Serikali, vyama vya siasa, Asasi za kiraia, wanaharakati na viongozi wa dini.
Akizitaja sheria na kanuni zinazoendelea kufanyiwa marekebisho ni pamoja na Political Parties Act (2019), Political Parties Code of Conduct (CAP.258 R.E.2019), Regulation of 2019, na Kanuni za maadili ya vyama vya siasa na kanuni nyenginezo, marekebisho hayo yatakapo kamilika yanatarajiwa kuondoa unyanyasaji kwa wanawake katika kushiriki masuala ya kisiasa.
Afisa sheria mwandamizi, alisisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni jambo lisilopingika, hivyo ni muhimu kwa vyama vya siasa kuzingatia hilo kwa kuandaa miongozo imara itakayosimamia maadili na kukemea vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake, sambamba na kuunga mkono wanasiasa wanawake, wagombea, wapiga kura ambao wanaweza kukabili vitisho, vurugu, kashfa na dhihaka kutokana na jinsia zao katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Mapema akimkaribisha Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, na Watoto, Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Dkt Mzuri Issa amesema kumekuwa na malalamiko ya wanawake kudhalilishwa wakiwa katika haraki za ushiriki wao katika siasa na hakuna mifumo mizuri ya kuripoti matukio hayo na upatikanaji wa haki
Nae Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee, na Watoto Mhe Anna Athanas Paul, amesema Wizara hiyo imeandaa mikakati maalum ikiwemo kutoa mafunzo, nyenzo na programu za ushauri ili kusaidia wagombea wanawake.
Tathmini ya vikwazo kwa wanawake katika kushiriki kwenye siasa na demokrasia imefanywa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Kitaifa la Kidemokrasia (NDI) na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Imetolewa na Kitengo cha Habari
TAMWA – Zanzibar.
Social Plugin