TAWA YATAKIWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU KATIKA UTENDAJI KAZI



Na Happiness Shayo -Morogoro

Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wmetakiwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo katika kuongeza tija na kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka hiyo.

Rai hiyo imetolewa leo Julai 8,2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika kikao chake na Menejimenti ya TAWA kilichofanyika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro.

Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kutoa onyo kwa Askari Uhifadhi wanaofanya vitendo visivyofaa katika maeneo yao ya kazi na kuelekeza wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.

"Tujitahidi kudhibiti vitendo visivyofaa kwenye maeneo yetu, pasiwe na uvamizi wa aina yoyote" amesisitiza.

Aidha, Waziri Kairuki ameonya tabia ya watumishi wanaochelewesha huduma kwa wadau.

"Kila mmoja akajichunguze wapi ameshiriki katika kuchelewesha utoaji huduma na kutofuata taratibu hasa katika utoaji wa vibali na nambari za malipo,” ameongeza.

Kuhusu minada ya vitalu vya uwindaji, Mhe. Kairuki amewataka kufanya minada hiyo kwa wakati kwa kufuata kalenda na pia kujifunza kutokana na matokeo ya minada iliyopita kama kulikuwa na changamoto waangalie namna ya kuzitatua , nini cha kuboresha na hadhi za vitalu wanavyovinadi ili kuongeza mapato ya Serikali.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki ameitaka TAWA kuwa na mpango mkakati wa kuongeza makusanyo kwa kunadi maeneo yao ya uwekezaji kwenye maonesho wanayoshiriki huku Wizara ikiendelea na mchakato wa kurekebisha kanuni mbalimbali na masuala ya tozo.

Pia Waziri Kairuki ameitaka menejimenti ya TAWA kuwa na utaratibu wa kujengea uwezo watumishi ili waweze kutimiza wajibu ipasavyo katika kuimarisha ulinzi ,doria na kupambana na ujangili katika maeneo ya hifadhi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA,Mabula Misungwi Nyanda, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Fortunata Msoffe, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wizara ya Maliasili na Utalii, Lucy Saleko.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post